Mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na marudio ni Mei 17 nchini Afrika Kusini.
Yanga imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuitoa Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0. Yanga ilianza kwa ushindi wa 2-0 ugenini na baadaye suluhu kwenye dimba la Mkapa.
Matokeo hayo yakaifanya Yanga isonge mbele na kujiwekea historia yake ya kutinga kwa mara ya kwanza hatua ya nusu fainali ya kombe hilo na sasa ina kibarua cha kuivaa Marumo.
Yanga ambayo kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ikiwa inahitaji pointi tatu tu kutangazwa kuwa mabingwa wapya, tunaamini kwamba wana kikosi kizuri chenye uwezo wa kuitoa Marumo na kutinga fainali.
Tunasema hivi kwa sababu ya ubora wa kikosi chenyewe cha Yanga ambacho kinanolewa na Kocha Nasreddine Nabi raia wa Tunisia akisaidiwa na Cedric Kaze, huku pia wakiwa wametinga nusu fainali nyingine ya Kombe la Shirikisho Tanzania (FA).
Tunafahamu kwamba, Yanga imefika hatua hiyo kutokana na kujituma kwa wachezaji wake, pamoja na ubora wa benchi lake la ufundi, hivyo tunaamini kabisa sasa ni wakati wa kuonesha kiwango kingine bora zaidi kwenye hatua hiyo.
Wapinzani wao Marumo hivi sasa wanapigania kutoshuka daraja kwenye Ligi Kuu ya nchini kwao Afrika Kusini na mwishoni mwa wiki (Jumamosi), walikutana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mamelod Sundown, hivyo Yanga wakitumia udhaifu wa timu hiyo vizuri wana nafasi kubwa ya kuwatoa na kutinga fainali.
Tunaamini kwamba, timu yoyote inapocheza kwenye dimba lake la nyumbani ina nafasi nzuri zaidi ya kupata matokeo chanya na hivyo kujiweka kwenye wakati mzuri zaidi katika mchezo wa marudiano ugenini.
Hivyo Yanga inapaswa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani wa Mkapa kuhakikisha inaibuka na ushindi wa mabao mengi, ili kurahisisha kazi kwenye mchezo wa marudiano.
Iwapo Yanga itapata ushindi wa mabao mengi itakuwa imejirahisishia kazi kuelekea mchezo wa marudiano, kwa sababu kazi kubwa watakayokuwa nayo ni kupambana kupata sare yoyote ili kutinga fainali.
Hata hivyo, pamoja na kwamba, wapinzani wao Marumo wanapambania kutoshuka daraja kwenye Ligi Kuu ya nyumbani kwako Afrika Kusini (ipo nafasi ya 14 katika timu 16 na pointi 29), lakini Yanga hawapaswi kuwabeza hata kidogo.
Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, licha ya kuwa na matokeo mabaya kwenye ligi ya nyumbani, lakini Marumo imeoneshwa kiwango bora na cha kuvutia kwenye michuano hii ya Shirikisho.
Ikimbukwe kwamba, Marumo hawa waliwalazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Pyramids ya Misri ugenini kabla ya kushinda bao 1-0 nyumbani na kutinga hatua hiyo iliyopo sasa.
Hivyo basi, Yanga wanatakiwa kuingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa sana, kwani wapinzani wao hawatabiriki, masihara au umakini mdogo unaweza kuwafanya wawe na wakati mgumu.
Tunaamini benchi la ufundi la Yanga limeifuatilia kwa ukaribu na umakini mkubwa michezo yote ya Marumo na kwamba hivi sasa wanajua ubora na udhaifu wa kikosi hicho.
Sisi Nipashe tukiwa kama mdau namba moja wa mchezo wa soka la michezo yote kwa ujumla, tuna imaini kubwa na Yanga na hivyo tunawatakia kila la heri kwenye mchezo wao huo na tunaamini hawatawaangusha Watanzania kwa sababu wanaliwakilisha Taifa.









