Kilio mchakato Katiba mpya kimesikika

09May 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kilio mchakato Katiba mpya kimesikika

HATIMAYE kile kilio cha kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya kimeanza kupata jibu baada ya mwishoni mwa wiki, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kumwagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi, kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu,

lengo ni kuwashirikisha wadau katika kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Imeelezwa kuwa Rais Samia ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kilichofanyika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali kuhusu kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.

Kikao hicho kimejadili namna ya kushirikisha wadau mbalimbali na hasa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato huo kutoka pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar.

Mbali na mchakato huo wa Katiba mpya, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi; zikiwamo Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro na watendaji wa taasisi mbalimbali.

Tunasema hatua hii iliyochukuliwa na Rais Samia, inarejesha matumaini ya kuanza mchakato huo ambao umekuwa kilio kikubwa cha Watanzania cha kutaka Katiba mpya.

Vyama vya siasa hasa vya upinzani ndiyo kimekuwa kilio chao katika mikutano yao ya kutaka Katiba iliyopo sasa ifanyiwe marekebisho ili iweze kutoa haki sawa kwa Watanzania wote na kuondoa sheria zinazoonekana kuwa na upungufu na kulalamikiwa na watu wengi.

Rais Samia anarejesha imani kwa Watanzania ya kuwapo na matumaini ya kupata Katiba mpya, ikizingatiwa kuwa wakati mchakato huo ulipoanzishwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, mwaka 2014 yeye (Rais Samia) ndiye aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mwenyekiti akiwa Samuel Sitta (marehemu).

Hata hivyo, mchakato huo hakuweza kufikiwa lengo lake, baada ya baadhi ya vyama vya upinzani kujitoa na kuanzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Licha ya kujitoa, Mwenyekiti wa Umoja huo, Freeman Mbowe, alisema wataendelea kushiriki kwenye vikao, ingawa wataendelea kupigania mageuzi ya msingi uendeshaji wa Bunge hilo ambalo lilitakiwa kutoka na Katiba mpya itakayopigiwa kura ya maoni ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili katika kipindi hicho cha mchakato.

Jaji Joseph Warioba, ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba. Bunge hilo la kwanza la aina yake ndani ya kipindi cha miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.

Mchakato wa kupata Katiba mpya ulikwama baada ya kikao cha Bunge Maalum la Katiba, kuahirishwa mara kadhaa na dalili zikionesha kuwapo hali ngumu na uwezekano wa kufikia muafaka kwa hatima ya Taifa la Tanzania.

Hatua ya Rais Samia sasa imefungua nuru mpya, Mungu ibariki Tanzania iweze kusonga mbele.