Waliohusika na fedheha hii wasionewe huruma asilani

04May 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waliohusika na fedheha hii wasionewe huruma asilani

KATIKA moja ya habari kwenye gazeti hili ni kutelekezwa kwa zaidi ya wafanyakazi na wanachama 70 wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) baada ya kumalizika kwa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Wanachama hao, kwa mujibu wa taarifa hiyo, walitarajia kulipwa posho ambazo pia zingewasaidia kupata chakula kutokana na kuhudhuria maadhimisho hayo kutoka kwa viongozi wa chama chao. Kinyume cha matarajio hayo, walijikuta wamebaki uwanjani wasijue la kufanya baada ya viongozi wao kuingia mitini.

Miongoni mwa wafanyakazi hao waliotelekezwa ni watendaji wa vijiji na kata, maofisa kilimo na wa idara ya afya. Hata baada ya kumalizika kwa sherehe hizo, walipotakiwa waondoke uwanjani hapo na kurejea nyumbani, waligoma huku wakitaka viongozi wao wawalipe ndipo watawanyike. Walikubali kuondoka baada ya viongozi wa TALGWU mkoa na wale wa serikali kuingilia kati.

Watumishi hao, wakizungumza na vyombo vya habari, walisema viongozi wao waliwatoroka na kuwaacha bila kuwapa nauli za kurudi kwenye vituo vyao vya kazi ilhali wenzao wa wilaya zote za mkoa wa Mbeya walilipwa.

Kitu cha kushangaza na kuonyesha viongozi hao hawana hata chembe ya huruma ni pale walipoondoka eneo la sherehe na kuzima simu zao. Hatua hiyo ilionyesha ni unyama uliopitiliza dhidi ya binadamu wenzao ambao ni wanachama wanaochangia mfuko wa chama kutoka kwenye mishahara yao ya kila mwezi.

Mmoja wa wanachama hao, alikaririwa na waandishi wa habari akisema viongozi hao waliwaahidi kuwa kila atakayehudhuria atalipwa posho na kupewa chakula cha mchana. Swali la kujiuliza ni je, nini sababu ya viongozi hao kuondoka na fedha ambazo ni haki ya wafanyakazi ambao wamekuwa wakichangia kutoka kwenye vipato vyao?

Lakini pia jambo la kushangaza, kama alivyosema mwanachama huyo ni kwamba kila mwaka wanapohudhuria sherehe hizo, wamekuwa wakilipwa Sh. 2,500. Ni hali mwanachama anayechangia sehemu ya mshahara wake kupewa kiasi hicho cha fedha? Je, mamilioni ya fedha yanayochangwa na kubaki katika wilaya husika yanafanya kazi gani?

Kwa ujumla, kitendo kilichofanywa na viongozi hao wa TALGWU wilaya ya Mbeya ni cha fedheha na udhalilishaji ambacho kinapaswa kukemewa na kulaaniwa na chama hicho ngazi ya mkoa na taifa pamoja na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Ni imani kwamba viongozi waliohusika na udhalilishaji wa wafanyakazi ambao huwakiwa na jua au kunyeshewa na mvua wakati wa maadhimisho hayo, watachukuliwa hatua na viongozi wao ngazi za juu ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo na wale wanaotafuna fedha za michango ya wafanyakazi kwa ajili ya maendeleo ya taasisi.

Pamoja na hayo, kitendo hicho kimedhihirisha kuwa baadhi ya viongozi wanaoingia kwenye vyama vya wafanyakazi, hawana nia thabiti ya kutetea maslahi ya wafanyakazi ambayo yamekuwa kilio kila mwaka wakati maadhimisho hayo yanapofanyika bali kinachowasukuma ni maslahi yao binafsi.

Aidha, kitendo hicho kimefumbua macho wadau wengi wa masuala ya wafanyakazi na nchi kwa ujumla kuwa unapaswa kufanyika ukaguzi wa fedha na mali za vyama hivyo, ikiwezekana kazi hiyo ifanywe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Ni imani kwamba iwapo kazi hiyo itafanyika, yataibuliwa madudu mengi yanayoweza kuwaanika wahusika na wengine kufikishwa katika vyombo vya sheria.