Wananchi wachukue hadhari matumizi ya vinywaji ‘energy’

25Apr 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wananchi wachukue hadhari matumizi ya vinywaji ‘energy’

VINYWAJI vya kuongeza nguvu, maarufu kama ‘enegy’, vimekuwa vikishabikiwa sana na watu wa marika mbalimbali nchini na kuvitumia kama sehemu ya kuondoa uchovu mwilini au kuchanganya na vinywaji vikali kwa kile kinachodaiwa ni kupunguza mning’inio na kutopata usingizi.

Kwa kupanda chati huko, kampuni mbalimbali nchini zimekuwa zikitengeneza bidhaa hiyo kutokana na kupendwa huku vingine vikiagizwa kutoka nje. Watumiaji wakubwa wa vinywaji hivyo ni madereva wakiwamo wa mabasi ya abiria ndani ya miji, maarufu kama daladala na wale wa mabasi na magari makubwa ya safari ndefu kwa kile kinachoelezwa kuwa kinawafanya wasichoke wakiwa kazini.

Watumiaji wengine wa kiwango cha juu cha ‘energy’ ni wanamichezo kwa kuamini kuwa wanapofanya hivyo wana uwezo wa kupata nguvu wakati wa mchezo. Kutokana na kuchangamkiwa na watu kwa kiasi kikubwa, hivi sasa katika maduka makubwa, madogo na sehemu za starehe kama hoteli na baa, vinywaji hivyo vinapatikana kwa wingi na vinanunuliwa kwa kasi.

Tayari serikali imeshaonya juu ya matumizi ya vinjwaji hivyo kutokana na kuwa na madhara makubwa ya afya. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeshaonya matumizi hayo kutokana na kupokea wagonjwa wengi wenye maradhi ya moyo ambayo historia yao inahusishwa na matumizi ya ‘enegy’.  Kwa mujibu wa taasisi hiyo, wagonjwa wengi wamekuwa wakifika kwa matibabu, wengi wakiwa na historia zinazofanana za matumizi ya vinywaji hivyo.

Wataalamu wa JKCI wamebainisha kwamba matumizi ya ‘energy’ yana athari kubwa kiafya kwa kuwa mtu anapotumia, baada ya dakika kadhaa caffeine huingia kwenye mzunguko wa damu hivyo kusababisha mtu kupatwa na shinikizo la damu na mapigo ya moyo kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida.

Hivi karibuni, mathalan, katika taasisi hiyo ilielezwa kuwa kijana wa miaka 21 alifikishwa hospitali akiwa na hali mbaya na baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa  alizidisha matumizi ya kinywaji hicho. Kwa mujibu wa taarifa hiyo kijana huyo alikuwa na maumivu makali ya kifua upande wa kushoto ulipo moyo na uchunguzi ulibaini kwamba alipatwa na matizo hayo kutokana na utumiaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu na kuwa kwa siku sita alikuwa amekunywa makopo matano kila moja likiwa na ujazo wa milimita 250.

Kama vile haitoshi, kijana huyo inasemekana alikuwa amekunywa lita moja na robo ya kinywaji hicho ndani ya saa nne na baada ya kumaliza kopo la mwisho, ndipo alipopatwa na mkasa huo na hatimaye kwenda hospitalini. Matumizi hayo ya kinywaji yalisababisha mishipa ya moyo kuziba, upande wa kushoto ukiziba kwa asilimia 100 na kama hali hiyo ingeendelea kwa saa kadhaa, misuli ya moyo ingekufa na hatimaye kukumbwa na kifo cha ghafla.

Kuwapo kwa taarifa hiyo, kumesababisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kuiagiza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya uchunguzi zaidi kuhusu matumizi ya vinywaji hivyo ili kupata ushahidi wa kisayansi.

Pamoja na serikali kuagiza uchunguzi kufanyika, ni vyema wanaotumia vinywaji hivyo, wakiwamo vijana na makundi yaliyotajwa, kuchukua tahadhari ili kuepukana na madhara yanayoweza kuwapata.