Kwenye nyumba za ibada viongozi wa dini huchukuliwa na waamini wao kama watu waliotumwa na Mungu kuja kuwafundisha matendo mema na kuyafuata.
Kwa sababu hiyo, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amewataka viongozi hao wasimamie haki na kuienzi kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Amewataka viongozi wa dini kukumbusha mara kwa mara waamini na watu wote kuhusu umuhimu wa kusimamia haki na kudumisha amani na kuiombea nchi na viongozi wake.
Rai hiyo ya Waziri Mkuu inakuja huku nchi ikiwa katika wimbi zito la binadamu kukiuka uumbaji wa Mungu na kwenda kinyume.
Wanaume sasa wanajigeuza na kuwa wanawake ili waolewe na wanaume wenzao na wanawake wanajigeuza na kutaka kuwa na misuli kama ya wanaume ili waweze kuoa wanawake wenzao.
Vitendo hivi vimeshamiri kutoka kwa watu wazima na sasa vinapelekwa kwa watoto ambao wanafundishwa kwenye baadhi ya shule, hali inayoleta hofu kubwa ya mporomoko wa maadili.
Serikali inachukua nafasi yake kukemea hali hii, taasisi mbalimbali zinakemea, lakini viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kukemea kwa sababu wanasikilizwa na wanaaminiwa kwa wanachokisema.
Kwenye nyumba za ibada iwe misikitini, kwenye makanisa iwe ajenda kwa viongozi hao kila wanapokutana na waamini wao kukaripia na kulaani.
Shule zinazofundisha watoto masuala dini nazo zina mchango mkubwa wa kukemea vitendo hivyo na walimu wanaogeuza shule hizo kuwa kichaka cha kuficha uovu wao hawana budi kuchukuliwa hatua kali.
Waziri Mkuu amewataka viongozi wa dini nchini kutochoka kufundisha na kulea vijana katika maadili mema na kuthamini kufanya kazi halali.
"Katika nyakati hizi ni ukweli ulio wazi kuwa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii yetu, vitendo viovu na mambo yasiyompendeza mwenyezi Mungu yanazidi kuongezeka, mambo ambayo siku za nyuma yalikuwa nadra sana kutokea au kusikia, lakini sasa yanakuwa habari za kila siku na wakati mwingine huonekana eti ya kawaida," anasema Majaliwa.
Kushuka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na taifa kwa ujumla na kunachangia kurudisha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo na kuifanya kazi ya kuondoa umaskini kuwa ngumu.
Anaamini kwa dhati kuwa viongozi wa serikali, dini na vyama vya siasa wakishika mafundisho ya dini na kuwa na hofu ya Mungu maovu mengi yatapungua na nchi kuongozwa vizuri.
"Naendelea kuwaomba kwa niaba ya serikali, viongozi wa dini zetu zote tusaidiane kuokoa taifa letu kimaadili na tuweke mkazo zaidi kwa vijana kwa sababu kwanza wao ndiyo wahanga wakuu wa maovu yanayotendeka, lakini pia wao ni taifa la leo na viongozi wa kesho."
Waziri Mkuu pia alisisitizia suala la elimu na kueleza kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote na kutaka viongozi wa dini kusaidia kuzungumza na wazazi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kusomesha watoto.









