'Dabi' Simba, Yanga imepita, akili zihamie robo fainali CAF

17Apr 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
'Dabi' Simba, Yanga imepita, akili zihamie robo fainali CAF

HATIMAYE mechi ya watani wa jadi 'Dabi' ya Kariakoo kwa timu kongwe zaidi nchini, Simba na Yanga, imepigwa jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni ya mzunguko wa pili baada ya ile ya raundi ya kwanza miamba hiyo kutoka sare ya bao 1-1 uwanjani hapo.

Miamba hiyo ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la nchi hii, imetinga kwa pamoja robo fainali ya michuano ya kimataifa kwa msimu mmoja, ina kibarua kigumu kuelekea mechi zao zijazo kuweza kusaka tiketi ya kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba inayoiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa, itaikaribisha Wydad Casablanca ya Morocco katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali utakaopigwa Jumamosi wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Makapa.

Kwa upande wa Yanga yenye kibarua cha kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, itakuwa na shughuli pevu ugenini nchini Nigeria Jumapili wiki hii dhidi ya wenyeji wao, Rivers United katika mechi ya mkondo wa kwanza ya hatua ya robo fainali.

Ni mechi ambazo mashabiki wa soka wa timu hizo, lakini kwa kila Mtanzania mwenye mapenzi mema ya kuona mpira wa nchi hii ukipiga hatua, anataka kuona wawakilishi hao wa nchi kimataifa kwa ngazi ya klabu, wakipata matokeo mazuri na kusonga mbele zaidi.

Kwa mantiki hiyo, bila kujali matokeo ya mechi ya jana, ni wakati wa kila mmoja hususan wachezaji na mabenchi yao ya ufundi, kuyasahau na kuelekeza akili zao kwenye michuano hiyo ya kimataifa ambayo inaongoza kwa utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Kwa muda huu wa takriban siku tano zilizosalia kabla ya wawakilishi hao wa nchi kushuka dimbani, ni wakati wa mabenchi yao ya ufundi si tu kuwapa mbinu wachezaji na kufanyia kazi kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza kwenye mechi zilizopita, bali kuwajenga zaidi kisaikolojia ili kuweza kupata ushindi.

Ingawa wapo wanaoona kuna mlima mrefu kwa Simba kuweza kupenya kutokana na kupangiwa Bingwa Mtetezi wa michuano hiyo, Wydad Casablanca, lakini pia wakiamini Yanga ina nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na ubora wa kikosi chao ukilinganisha na cha msimu uliopita ambacho kilitupwa nje na Rivers United kwenye Kombe la Shirikisho, lakini sisi hatuamini katika hilo kwani hatua kama hii timu zote ni bora.

Kadhalika, kwa Yanga kuamini tu wana kikosi bora pasipo kujipanga vizuri na kuwaheshimu Rivers United wakiwa kwao, wanaweza kujikuta wakibebeshwa mzigo mkubwa na mechi ya marudiano kuwawia vigumu 'kupindua meza'.

Aidha, ikumbukwe Rivers United hiyo, nayo ilianzia Ligi ya Mabingwa kabla ya kutolewa na Wydad Casablaca kwenye raundi ya kwanza, hivyo kuangukia Kombe la Shirikisho kama ilivyo Yanga ambayo iliondoshwa na Al Hilal ya Sudan, hivyo si timu ya kuibeza hata kidogo.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba ikiwa nyumbani katika mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Wydad iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 kabla ya kwenda kuangukia pua ugenini kwa kipigo cha mabao 6-0 nchini Morocco, hivyo Yanga inapaswa kujipanga vilivyo na si kuibeza.

Sisi tunaamini wawakilishi wetu hao, Simba na Yanga, wakijipanga vizuri na kucheza kwa kujiamini huku wakiwaheshimu wapinzani wao, wanaweza kabisa kupata matokeo mazuri na kusonga mbele nusu fainali na hata fainali, hivyo kwa siku hizi chache ni wakati wakusahau matokeo ya mechi ya jana na zilizopita na kisha kujipanga vema kwa mechi hizo za kimataifa.