Wakati ugonjwa wa UVIKO-19 ulipoingia nchini kwa kasi miaka miwili iliyopita, Tanzania ilihitaji vifaa tiba kwa wingi ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na kulazimika kuagiza kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji.
Siku zote panapojitokeza changamoto, ndipo watu hupata suluhisho la kupambana na kuja na jibu la kuondokana na changamoto hiyo.
Katika kupambana na changamoto ya kuagiza vifaa tiba kutoka nje, MSD imetaja hatua mbalimbali inazochukua ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda viwili vya barakoa na kimoja cha kuzalisha mipira ya mikono.
Idara ya Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji ya MSD, imeeleza sababu za bohari hiyo kuanzisha kampuni tanzu na viwanda vyake.
Katika viwanda hivyo, kiwanda cha kutengeneza barakoa kimejengwa jijini Dar es Salaam, eneo la Keko, wilayani Temeke na uwekezaji wake ni Sh. bilioni 1.4.
“Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha barakoa 80 kwa dakika, uwekezaji wake ni Sh. bilioni 1.4 ambacho kwa mwaka kinazalisha barakoa milioni 5.8, kilianza kazi Agosti 2020. Kiwanda hiki kinaonesha umuhimu wa viwanda, kilianza kazi wakati wa janga la UVIKO-19 na wakati ule haikuwa rahisi kupata barakoa.
“Kabla ya kuanzisha kiwanda hiki, barakoa moja ilikuwa ikiuzwa Sh. 1,600, lakini kwa sasa inauzwa Sh. 500, na uwapo wa kiwanda hiki umesaidia Tanzania kuacha kuagiza nje ya nchi na hivyo kiwanda kimepunguza matumizi ya fedha za kigeni.” MSD inafafanua
Kiwanda kingine cha kuzalisha barakoa ni cha N95 kilichozinduliwa rasmi Machi, mwaka huu, chenye uwezo wa kuzalisha barakoa 100 hadi 150 kwa saa moja.
Kuhusu kiwanda cha kuzalisha mipira ya mikono, kilichopo Idofi mkoani Njombe, kinatarajia kuanza uzalishaji Julai, mwaka huu na kitakuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji kwa asilimia 100.
“Kiwanda kitatoa ajira zaidi ya 200 za moja kwa moja na ambazo sio za moja kwa moja. Viwanda vyote hivyo vitaokoa fedha za kigeni na tunataka malighafi za viwanda hivi zitoke nchini. Tukifanikwa tutatengeneza mzunguko mzuri wa fedha na kuimarisha uchumi."
Hatua hii ya MSD sio tu inaokoa fedha za kigeni, bali pia inasaidia kupunguza tatizo la ajira linaloikabili nchi kutokana na vijana wengi kukosa ajira wamalizapo vyuo.
Viwanda hivyo vitasaidia kutoa ajira za kudumu na zisizo za kudumu na kupunguza tatizo la vijana wanaozagaa mitaani kutafuta ajira.
Vile vile, viwanda hivyo vitasaidia wakulima wa hapa nchini kwa sababu vitahitaji malighafi inayozalishwa hapa hapa na kuwakomboa kwa kipato.
Kwetu sisi tunasema hatua hii ni kubwa na muhimu, kwa kuwa hapo mwanzo barakao zilikuwa zikiagizwa kutoka nje na kuuzwa kwa bei kubwa tofuati na zitakazozalishwa nchini ambazo zitakuwa na gharama nafuu na kila mtu atamudu kununua.









