Katika mechi ya mkondo wa kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo kwenye mchezo wa keshokutwa, inahitaji sare yoyote ama kutoruhusu kufungwa zaidi ya bao moja au kupata ushindi wowote, ili kutinga fainali.
Hadi kufika nusu fainali, hiyo ni rekodi kubwa kwa Yanga kuweza kucheza hatua hiyo ya michuano ya CAF ikiwa ni mara ya kwanza tangu klabu hiyo imeanzishwa miaka 88 iliyopita, hivyo kama itafanikiwa kufika fainali, itaendelea kujiwekea rekodi zaidi.
Kwa ujumla, si mashabiki wa Yanga pekee wanaotaka kuona klabu hiyo ikitinga fainali, bali ni Watanzania wote kwa ujumla, wanapenda kuona hilo likitokea kwani haitakuwa heshima kwa timu hiyo pekee bali kwa soka la Tanzania kwa ujumla wake.
Tunasema hivyo hasa tukitambua kwamba mafanikio ya Yanga si tu yataitangaza klabu hiyo, bali soka la Tanzania litazidi kutangazika na kuvutia wachezaji wakubwa na hata wawekezaji zaidi, jambo ambalo litaongeza kipato kwa wachezaji na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Hivyo, ili hilo litokee, juhudi zinahitajika kwa wachezaji wa Yanga, benchi la ufundi na viongozi kwa ujumla kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kwenda kumalizia kazi nzuri waliyoianza tangu kuanza kwa msimu wa michuano hiyo inayoratibiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF.
Tunaamini Yanga wamejiandaa vizuri na wanaendelea kujiandaa kwenda kupata matokeo chanya ama kulinda ushindi walioupata nyumbani ili kutinga fainali na hata kuchukua ubingwa wa michuano hiyo ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tunatambua hautakuwa mchezo rahisi pale katika Uwanja wa Royal Bafokeng, Afrika Kusini, lakini kwa ubora wa Yanga ambao wamekuwa wakiuonyesha katika michuano hiyo nyumbani na ugenini msimu huu, hatuna shaka katika hilo.
Kikubwa ni kila mchezaji kubeba jukumu lake ipasavyo, akitambua kwamba mafanikio katika michuano hiyo si sifa tu kwa klabu, bali pia ni daraja pekee kwake katika kutangaza kipaji chake na kujitafutia soko kwa klabu kubwa nje ya nchi.
Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba katika michuano hiyo, mawakala wengi hutupia macho hususan kwa klabu zinazofika hatua za juu kama hiyo, jambo ambalo halitashangaza kuona baadhi ya wachezaji wa Yanga wakipata soko kwenda klabu kubwa zaidi baada ya kutamatika kwa mashindano hayo.
Tunaamini katika kipindi hiki kichache kilichobaki, benchi la ufundi la Yanga pamoja na kuendelea kuwapa wachezaji mbinu za kiufundi, lakini pia watakitumia kuwaandaa kisaikolojia ili wakiwa ugenini wasione tofauti yoyote na wacheze kwa kuufurahia mchezo kama wapo vile wakiwa nyumbani bila kujali mchezaji wa 12, ambaye ni mashabiki wa timu mwenyeji.
Nipashe tunaitakia Yanga maandalizi mema na safari njema na matarajio yetu makubwa ni kuona ikirejea nchini na rekodi yao mpya ya kutinga fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.