Mpaka sasa tayari wizara kadhaa zikiwamo ofisi za Rais na Waziri Mkuu zimeshawasilisha makadirio yao. Baada ya kukamilika kwa makadirio ya wizara hiyo, ndipo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, atawasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha ambayo itaweka bayana vipaumbele kwa mwaka husika na maeneo ya vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia katika utekelezaji wa bajeti hiyo ikiwamo miradi ya maendeleo.
Sambamba na wabunge kujadili na kupitisha makadirio ya wizara hizo, pia wanapata nafasi ya kuuliza maswali ili kupata majibu ya kero zilizoko kwenye majimbo yao na sehemu zingine. Aidha, kila Alhamisi, wabunge wanapata fursa ya kumuuliza maswali Waziri Mkuu ambayo mengi ni ya kisera zaidi.
Wakati yote hayo yakiendelea, wiki hii, Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, alifanya kituko cha mwaka wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa kile alichodai ni kutokuridhishwa na majibu ya swali alilouliza. Mbunge huyo ambaye ni kipindi chake cha pili na alishakuwa Naibu Waziri katika serikali ya awamu ya tano, alivua tai na koti kisha akatoka nje.
Hatua hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Tulia Ackson, kupokea mwongozo na kulitolea majibu suala hilo huku akisisitiza kwamba kanuni za kudumu za bunge haziruhusu mbunge kuvua nguo akiwa bungeni na kuweka bayana kwamba kitendo alichofanya Waitara ni cha utovu wa nidhamu. Bila kuuma maneno, Dk. Tulia aliweka bayana kuwa kanuni za bunge hazitoi nafasi asilani kwa mbunge kufanya kituko cha aina yoyote kama alivyofanya Waitara.
Kitendo alichokifanya mbunge huyo kimeonyesha ni namna gani wabunge wanavyokiuka kanuni na miongozo iliyowekwa katika kuwasimamia wawapo katika chombo hicho kwa ajili ya kuwawakilisha wapigakura wao kujadili na kuzitafutia ufumbuzi kero zinazowahusu wananchi katika maeneo yao ya uwakilishi.
Kwa kawaida, mbunge anapouliza swali la msingi na kujibiwa na serikali, ana nafasi ya kuuliza angalau maswali mawili ya nyongeza ili kupata undani wa kile anachotaka. Waitara badala ya kufanya hivyo, aliamua kuvua koti na tai na hatimaye kwenda nje ya ukumbi wa bunge. Kwa ujumla, kitendo hicho kimeonyesha baadhi ya wabunge wanavyoshindwa kusimamia kanuni zinazowaongoza ambazo wamezitunga wenyewe.
Miaka kadhaa iliyopita, wananchi waliliona bunge ni kama sehemu ya watu kupiga porojo na kufanya mipasho kutokana na vijembe vilivyokuwa vimetawala wakati wa shughuli mbalimbali za chombo hicho. Kwa kilichotokea wiki hii, kimesadifisha dhana hiyo na kuwafanya baadhi ya wananchi kuamini kwamba wabunge wanaingia katika mhimili huo wa kutunga sheria kwa maslahi binafsi.
Bunge ni chombo kinachoheshimika kutokana na nafasi yake katika mwelekeo na hatima ya nchi kwa sababu ndiyo taasisi ambayo imepewa jukumu la kutunga sheria, kupitisha bajeti na kuishauri serikali juu ya masuala yanayopitishwa. Sasa kama bunge lenyewe haliwezi kusimamia kile ilichokitunga. Watu wengine watakuwaje radhi kutekeleza maelekezo na maazimio yake?
Kuwapo kwa vitendo kama hivyo kunadhihirisha wazi kutokuwapo kwa umakini kwa baadhi ya wabunge na matokeo yake kushindwa kutunga sheria nzuri kwa maslahi ya taifa. Pia kitendo kama cha Waitara, kinaibua maswali mengi ikiwamo kama ni kweli huwa wanakaa, kusoma na kupitia kwa kina masuala yanayowasilishwa ikiwamo miswada ya sheria ili kutoka na sheria bora badala ya bora sheria?.