Elimu matumizi sahihi ya dawa iendelee kutolewa

11May 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Elimu matumizi sahihi ya dawa iendelee kutolewa

MARA kwa mara wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza watu kuacha kuchukua uamuzi wa kumeza dawa au kufanya jambo lolote pindi wanapohisi dalili zisizo za kawaida katika miili yao.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba baadhi ya watu wanapojihisi homa au kuwa na dalili za malaria, kwa mfano, hukimbilia kumeza dawa. Hatua hiyo wakati mwingine imekuwa ikisababisha maradhi na madhara mengine yakiwamo kuibuka kwa magonjwa kama saratani au kutengeneza sumu mwilini kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Katika kampeni kama hizo, iko moja inayosisitiza kuwa si kila homa ni malaria hivyo mtu anapojihisi hali tofauti katika mwili wake, asitumie dawa na badala yake aende katika kituo cha kutolea huduma za afya na kufanyiwa vipimo hatimaye kupewa dawa zinazostahili kwa ugonjwa aliobainika kuwa nao.

Licha ya watu hao kuchukua uamuzi huo, wamiliki wa maduka ya dawa au wafanyakazi wao wamekuwa wakielekezwa mara kwa mara kutotoa dawa kwa mtu yeyote bila kuwa na cheti cha daktari au kuwaandikia matibabu kwa kuwa hawana fani ya utabibu.

Pamoja na msisitizo huo, wako watu ambao wameendelea kufanya hivyo kwa kumeza dawa au kwenda kwenye maduka ya dawa na kuwaeleza wauzaji kisha kupewa dawa na kuzimeza. Hali hiyo, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa na wataalamu na viongozi wenye dhamana katika afya, ina athari kubwa kwa wale ambao wamekuwa wakipuuza maelekezo hayo.

Hivi karibuni kwa mfano, mkoani Arusha, mwananchi mmoja ameripotiwa kuwa ameoza vidole vitano vya mkono baada ya kudaiwa kuchomwa sindano katika duka la dawa baada ya kuelezwa kuwa ana maambukizi katika njia ya mkojo (UTI). Ilidaiwa kuwa vidole hivyo vya mkono wa kushoto viliungua kwa kubadilika rangi na kuwa vyeusi muda mfupi baada ya kuchomwa sindano hiyo mkononi.

Baada ya kupatwa na tatizo hilo, mtu huyo alipelekwa katika hospitali ya rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi na kubainika kuwa vidole hivyo vimeharibika, hivyo anatakiwa kukatwa kwa kuwa vimeoza baada ya damu kushindwa kufika katika eneo hilo kutokana na mishipa inayosambaza damu kuziba.

Wataalamu wa afya katika hospitali hiyo, akiwamo daktari bingwa aliyemfanyia uchunguzi na kutoa uamuzi wa kukatwa vidole hivyo, kama ilivyo ada, walitoa tena angalizo kuwataka watu kuacha kuchukua uamuzi wa kutumia dawa au kupata huduma katika sehemu zisizostahili zikiwamo maduka ya dawa.

Pamoja na ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya juu ya matumizi sahihi ya dawa, jambo hilo limeonekana kama linaingilia upande mmoja wa sikio na kutokea upande wa pili. Kwa maneno mengine, watu hao ambao wamekuwa wakipuuza ushauri huo, wamekuwa kama sikio la kufa ambalo katu halisikii dawa.

Kwa ujumla, kuna athari kubwa katika utumiaji wa dawa bila kufuata ushauri wa kitabibu kutoka kwa madaktari. Miongoni mwa athari hizo ni dawa hizo kutengeneza sumu katika mwili na kusababisha baadhi ya viungo muhimu katika mwili wa binadamu vikiwamo figo, moyo na ini kuharibika. Wakati mwingine, dawa hizo zinapoingia mwilini na kushindwa kutibu ugonjwa usiohusika, mtu anaweza kupata maradhi makubwa kama saratani.

Ni vyema wataalamu wa afya chini ya Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, wakatoa elimu zaidi juu ya matumizi sahihi ya dawa ikiwamo kutumia zile ambazo wameandikiwa na madaktari katika vituo vya huduma za afya baada ya kufanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa na ugonjwa halisi.

Hali hiyo, ni dhahiri kwamba itaepusha matatizo mengi yanayoweza kujitokeza na hatimaye kuwaponyesha maelfu ya Watanzania.