Matukio hayo ni mwananchi mmoja kujirusha kutoka ghorofa ya saba katika jengo la Derm Plaza, Kijitonyama na kupoteza maisha na lingine ni watu saba kujeruhiwa katika jengo la Millennium Tower, Makumbusho.
Majengo hayo yanatazamana na yako kando ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Haijafahamika sababu za kijana huyo ambaye pamoja na mambo mengine alikuwa mshereheshaji (MC) kujitoa uhai. Lakini sababu ya watu waliojeruhiwa kwenye lifti ni kwamba chombo hicho ambacho hupandisha na kushusha watu kilikosa breki. Sambamba na kukosa breki, ilielezwa kuwa lifti hiyo ilikuwa katika matengenezo na kwamba haikujaribiwa kama imeimarika kabla ya kuruhusu watu kuipanda.
Kwa mujibu wa wataalamu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, lifti hiyo haikutakiwa kubeba watu kabla ya kujihakikishia kuwa ina uwezo na badala yake wasimamizi walipaswa kuijaribisha kwa kushusha na kupandisha mizigo, jambo ambalo halikufanyika.
Tukio la watu kujeruhiwa au kunasa kwenye lifti si la kwanza kutokea nchini bali ni la muda mrefu. Ziko taarifa zilizotolewa kuhusu lifti katika majengo mbalimbali kukumbwa na hitilafu, hivyo kusababisha watu kupata matatizo mbalimbali ikiwamo kukosa hewa na kujeruhiwa kama ilivyotokea juzi.
Mbali na lifti katika majengo, tatizo lingine ambalo limekuwa la muda ni vyombo vya moto hasa vya majini kwa maana ya vivuko kukumbwa na changamoto ya kuzimika na wakati mwingine abiria kukumbwa na taharuki wakiwa katika vyombo hivyo. Iko mifano mingi ya vivuko hivyo katika Bahari ya Hindi na maziwa kama Victoria na Tanganyika vyombo hivyo kupata hitilafu katikati ya safari.
Sababu za kutokea hitilafu hizo zikiwamo kuzimika kwa injini vikiwa na abiria ni kutokuwapo kwa ukaguzi, huduma (service) na matengenezo ya mara kwa mara ndiyo maana majanga kama hayo hutokea.
Hivi sasa kuna ongezeko la majengo ya ghorofa katika miji mikubwa, Dar es Salaam ikiwamo, hivyo ni vyema miundombinu kama lifti na umeme ikasimamiwa ipasavyo wakati wa ujenzi wake.
Hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupungua majanga yanayoweza kutokea na kusababisha maisha ya watu kupotea. Ni vyema mamlaka na taasisi zinazosimamia ujenzi na masuala ya ufundi zikawajibika ipasavyo ili kuhakikisha majanga yasiyo ya lazima yanaepukika.
Katika kuhakikisha hayo yanafanyika, kila hatua ya ujenzi na ukaguzi ufanyike kwa lengo la kujiridhisha kuwa masuala ya viwango yanafuatwa. Baada ya kukamilika, taasisi kama zimamoto na uokoaji, zifanye ukaguzi wa mara kwa mara ili kuona kama suala la usalama linazingatiwa kwa maana ya kuwa na vifaa vya kuzimia, mfumo imara wa umeme na kama majengo ni marefu lifti zinafanya kazi na zinafanyiwa ukarabati na matengenezo mara kwa mara.
Aidha, katika vyombo vya majini, Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA) ihakikishe vinakaguliwa mara kwa mara pamoja na kufanyikwa matengenezo. Ni Imani kwamba kwa kufanya hivyo, majanga mengi yanaweza kuepukika na kuwafanya wananchi na watumiaji wengine kuwa salama.
Wahenga wanasema ni heri kuzuia kuliko kutibu, hivyo kuwapo kwa ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara ya vyombo vya usafiri na lifti katika majengo, kutazuia kwa kiasi kikubwa majanga kama lile lililotokea juzi na kuzua taharuki miongoni mwa wananchi.