Alichokibuni DC wa Korogwe ‘Mamathon’ kiungwe mkono

30May 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Alichokibuni DC wa Korogwe ‘Mamathon’ kiungwe mkono

UBUNIFU wa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo, hauna budi kuungwa mkono na watu wote ili kunusuru wajawazito na changamoto za uzazi.

Mkuu huyo wa wilaya ameanzisha mbio za wajawazito zenye lengo la kuondoa changamoto wanazokutana nazo wakiwa katika hali hiyo na vile vile kuwaweka katika afya bora.

Alipotangaza kuanza kwa mbio hizo, aliomba kinamama wenye hali hiyo kujitokeza na kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki.

Kitu kilichotia moyo ni jinsi mwamko wa kinamama hao ulivyokuwa mkubwa na kufikia idadi ya wajawazito zaidi ya 2,000 waliojiandikisha.

Kilichopendeza zaidi ni jinsi kinababa nao walivyojitokeza kuwasindikiza kinamama hao katika mbio hizo.

Kwa kweli jambo hilo ni la kuungwa mkono na watu wote ili kulinda afya za wanawake wasikumbane na matatizo wakati wanapokwenda kujifungua.

Tumeelezwa kuwa wakati mbio hilo zikiendelea baadhi ya kinamama walikimbizwa hospitali baada ya kujisikia hali ya kutaka kujifungua.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mwanamke anapokuwa katika hali ya ujauzito anatakiwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara hasa ya kutembea, ili kupata urahisi anapofikia wakati wa kwenda kujifungua.

Mwili unapokuwa na mazoezi humsaidia mama kuondokana na shida zinazojitokea wakati anapokuwa na ujauzito.

Cha kuzingatia tu ni kwamba kabla ya kuanza mazoezi hayo ni lazima mtu afuate ushauri wa daktari ambaye atamwelekeza nini cha kufanya na nini asifanye.

Wakati DC akihamasisha mbio hizo, alisema wazi kuwa wajawazito wenye miezi ya karibu na kujifungua hawashauriwi kushiriki katika mbio hizo kwa sababu mama anaweza akapata athari ikiwamo kujifungua kabla ya miezi kutimia.

Sisi tunampongeza DC Jokate kwa ubunifu huo na ameonyesha jinsi anavyowajali wanawake wenzake hasa ikizingatiwa kuwa na yeye amepitia katika hali hiyo na sasa ni mama.

Hamasa iliyoonyeshwa na kinamama hao pia ni kuunga mkono ubunifu wa mkuu wao wa wilaya na kujiweka katika mazingira yenye afya bora katika kipindi cha ujauzito.

Ushauri wetu ni kuwa ubunifu huu ulioanzishwa na Jokate uigwe pia kwenye wilaya na mikoa mingine ili tuwasaidie kinamama wanaopitia changamoto za uzazi.

Sio kitu kibaya kuiga mazuri yaliyoanzishwa na kiongozi mmoja, kwa kuwa hiyo itaonyesha kuwa jambo hilo ni zuri na linapaswa kuendelezwa.

Mwenyewe Jokate akishiriki mbio hizo alisema lengo la kufanya tukio hilo ni kuenzi yale yote ambayo Rais Samia ameyafanya kwa ajili ya kusaidia wanawake na watoto.

Pia, katika mbio hizo walitoa masharti kwa wale wenye ujauzito wa miezi kuanzia nane wasihudhurie kwa sababu wapo katika hali ya kujifungua wakati wowote.

Katika mbio hizo wajawazito pia walipewa ushauri wa vyakula bora wanavyotakiwa kula wakati wakiwa katika hali hiyo ili kujenga afya ya mama na ya mtoto aliye tumboni.

Kwa hiyo, mbio hizo sio tu zinamsaidia mama kwa mazoezi bali pia zinatoa elimu ya vyakula anavyotakiwa kula akiwa katika hali hiyo.

Tunarudia kumpongeza Jokate kwa ubunifu huo na kuzidi kumtia moyo wa kubuni vingine vizuri zaidi kwa sababu ameonyesha kuwa ni jembe.