Mpango wa mafunzo JKT unapaswa kuungwa mkono 

31May 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mpango wa mafunzo JKT unapaswa kuungwa mkono 

HIVI karibuni, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilitangaza kuwa limeandaa mazingira ya kuwezesha vijana wote wanaomaliza kidato cha sita mwaka huu, kujiunga na mafunzo ya kijeshi kupitia taasisi hiyo.

Lengo la mafunzo hayo, kama ilivyo kwenye malengo la kuanzishwa kwake, ni kuwajenga vijana wa Kitanzania katika hali ya ukakamavu na uzalendo kwa nchi yao.

Tangu kuanza kwa jeshi hilo mwaka 1963, Watanzania wengi, wakiwamo wale wanaomaliza kidato cha sita na vyuo mbalimbali, walijiunga na jeshi hilo kwa mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa sheria. Mafunzo hayo yalianza kufanyika kwa miezi sita baadaye mwaka mmoja kabla ya kufutwa mwaka 1994 kutokana na sababu mbalimbali lakini yalirejeshwa miaka ya karibuni na kufanyika kwa miezi mitatu.

Viongozi mbalimbali wakiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mawaziri wakuu wa wakati huo, Edward Sokoine, Rashidi Kawawa na aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Chifu Adam Sapi Mkwawa, walijiunga na mafunzo hayo. Hiyo yote ilikuwa kuonyesha kuwa mafunzo hayo ni muhimu na kila Mtanzania hasa vijana wanaomaliza masomo kidato cha sita na vyuo wanajiunga.

Licha ya kufundishwa ukakamavu na hali ya kujiamini, Watanzania hao pia walifundishwa namna ya kujitambua katika kukabiliana na mazingira yanayowazunguka pamoja na kushiriki masuala ya kijamii na kujitegemea kimaisha.

Wakati wa mafunzo hayo, wale waliokuwa wamepitia mafunzo ya fani mbalimbali kama tiba, kilimo, mifugo  na ufundi, walipelekwa katika vitengo mbalimbali vinavyohusiana na fani zao. Waliokuwa wamemaliza kidato cha sita, walifanya kazi katika bustani, mashamba na mifugo na huko walipata maarifa ya namna mbalimbali za kufanya kazi kwa kujituma na kwa weledi.

Hata wale waliokuwa wametoka katika familia za watu mashuhuri na mambo yote yanafanywa na wafanyakazi wa ndani nyumbani kwao, walibadilika na kuwa wachapakazi wazuri, yote ikiwa ni kuwajenga kujitegemea katika majukumu mbalimbali watakapoingia katika ajira na maisha  kwa ujumla.     

Kimsingi, mafunzo hayo yalikuwa kama daraja la kuwafunza vijana namna ya kukabiliana na changamoto za kimaisha na wengi wao waliyamudu ndiyo maana waliokuwa wamepitia JKT, walipoingia katika kazi na kupewa majukumu mbalimbali, walionyesha uwezo mkubwa na kuleta tija kwenye taasisi walizofanya kazi.

Mpango huo wa JKT kuwataka vijana wote waliomaliza kidato cha sita na taaluma mbalimbali za ngazi ya cheti na diploma kujiunga na mafunzo hayo, umekuja wakati mwafaka kutokana na mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii ambayo kwa kiasi kikubwa yamechagizwa na mmomonyoko wa maadili.

Ni imani kwamba vijana hawa watakapojiunga na mafunzo hayo, bila kujali muda watakaotumia, watabadilika na kuwa watu wenye uzalendo na wenye kujitambua na kujiamini tofauti na ilivyo sasa katika makundi mbalimbali kutokana na kutojishughulisha na kazi mbalimbali za kujiingizia kipato. Matokeo yake vijana hao wamekuwa watu wa kukaa vijiweni na kutegemea vitu vya bure, jambo ambalo ni rahisi kuingia katika mitego ya kurubuniwa na kujihusisha na mambo maovu.

Ni ushahidi ulio wazi kwamba vijana wengi, hasa wa kiume, hivi sasa wameelekeza fikra katika michezo ya kamali, maarufu kama kubeti, badala ya kukijita kazi uzalishaji na kazi mbalimbali ambazo zitawaondoa katika utegemezi na lindi la umaskini.

Mpango wa JKT kuwachukua vijana wote waliomaliza elimu ya sekondari ya kidato cha sita na vyuo, unapaswa kuungwa mkono na wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kwa kuwa una nia njema kwa taifa  katika kurejesha uwezo wa vijana kujitambua na kutumia maarifa yao kwa maendeleo yao.