Hatua hiyo ya serikali inatokana na baadhi ya shule binafsi kuwazuia wanafunzi kwenda likizo nyumbani na kubaki shuleni, huku wakiendelea kuwatoza gharama za kubaki shule wazazi wa wanafunzi hao.
Baadhi ya shule hizo zimebainika kuwa zinachukua uamuazi huo bila kushauriana na wazazi wa wanafunzi hao, kitendo ambacho hakikubaliki.
Hali hii inaweza kusababisha mtoto akasingizia kutakiwa kubaki shuleni na kwenda kufanya mambo ya ovyo, huku mzazi akijua kuwa mtoto wake yuko shuleni.
Zuio hilo linatokana na malalamiko ya wazazi ambao watoto wao wamebaki shule hususan wa madarasa ya mitihani.
Serikali imezionya shule hizo na kuzitaka kuzingatia waraka uliotolewa na Kamishna wa Elimu.
“Kwa shule binafsi Kamishna alitoa unafuu kidogo kwamba waangalie ile kalenda, lakini wanaweza kufanya adjustment kulingana na mahitaji yao, ukweli unabakia palepale kwamba wanafunzi wetu wanahitaji kupumzika na baya zaidi kuna baadhi ya malalamiko tumeanza kupokea kwamba kuna shule zinazuia wanafunzi kwenda likizo bila hata kushauriana na wazazi na wengine wazazi wanatakiwa walipe kwa kuwaweka wanafunzi shuleni.”
Kwa shule za serikali kuna mwongozo umetolewa na Kamishna wa Elimu wa siku za kufunga shule na siku za kufungua ambao ni muhimu shule binafsi zikajifunza kuzingatia mwongozo na wanafunzi kupata fursa ya kupumzika.
Wakuu wa shule wote na wakurugenzi wametakiwa kuzingatia utaratibu huo na wito wa serikali ni kwamba shule hizo zisimlazimishe kamishna atoe waraka wenye masharti makali kwa sekta binafsi.
Wamiliki wa shule lazima wazingatie kuwa likizo zimewekwa kwa ajili ya wazazi kupata fursa ya kuwa na watoto wao kucheza na kubadilisha mazingira ambayo inawasaidia na wataalamu wa elimu wanajua kuwa ni muhimu kufanya hivyo.
Umuhimu wa likizo pia unamsaidia mzazi kuzungumza na mtoto wake, kujua changamoto zinazomkabili, maadili yake na vile vile kujua maendeleo yake kimasomo. Mtoto anapozuiwa kubaki shule, matokeo yake ni kumfanya mzazi na mtoto mwenyewe kushindwa kupeana taarifa.
Ndiyo maana baadhi ya watoto wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia wanashindwa kuwaeleza wazazi wao kwa sababu ya kukosa ukaribu wao.
Tamko hilo la serikali linazihimiza shule zizingatie agizo hilo na pale ambapo kuna makubaliano na wazazi kwa shule binafsi kwamba watoto wakae yawe makubaliano ya hiyari sio ya kulazimishana na pamoja na kuongeza muda kidogo kama wameamua kuongeza kwa ajili ya maandalizi, lakini lazima watoe muda kwa watoto, vilevile kwenda kupumzika.
Hata hivyo, Waziri anayehusika na elimu ameonya kuwa endapo malalamiko ya wazazi yataendelea, Kamishna wa Elimu atalazimika kutoa waraka. Cha msingi ni shule kuzingatia agizo lililotolewa ili zisilazimishe serikali kuchukua hatua kali na baadaye kuziathiri shule nyingine.
Mtoto lazima apewe haki yake ya kupumzika, anapohenyeshwa inaweza pia kumuathiri katika masomo na badala ya kumsaidia, ikamharibia.