Yanga inastahili pongezi kuiwakilisha vyema nchi

05Jun 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga inastahili pongezi kuiwakilisha vyema nchi

WAWAKILISHI wa Tanzania juzi walihitimisha safari yao ya kuwania kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya mchezo wa pili wa fainali uliochezwa kwenye Jiji la Algers, nchini Algeria.

Yanga licha ya kushinda kwa bao 1-0 ugenini bado matokeo hayo hayakuweza kuwapa nafasi ya kutangazwa mabingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Mei 28 jijini Dar es Salaam kufungwa mabao 2-1.

Ni kweli Yanga haijafanikiwa kutwaa ubingwa huo, lakini imeonyesha ushindani wa hali ya juu na kuitangaza nchi kwenye soka la Afrika.

Wapo watakaowabeza Yanga baada ya kushindwa  kutwaa ubingwa huo, lakini ukiwa mpenzi wa soka huwezi kubeza mafanikio waliyofikia Yanga msimu huu kwenye mashindano ya kimataifa.

Awali Yanga waliweka wazi malengo yao kwenye mashindano ya kimataifa hususani kwenye michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho baada ya kuondolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kupitia kwa Rais wake, Injinia Hersi Saidi, Yanga walikuwa na malengo ya angalau kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, lakini kujituma kwao na ubora wa kikosi chao wamefanikiwa kuvuka malengo yao na kucheza fainali ya michuano hiyo.

Tunafahamu upo ubishani na utani wa jadi, lakini Yanga wanastahili pongezi nyingi baada ya kufika fainali na kuonesha ushindani mkubwa dhidi ya klabu kubwa ya USM Algers.

Kile walichokifanya Yanga kila mpenzi wa soka katika nchi hii na hata nje ya Afrika amekiona na ataungana na sisi kuwapongeza kwa soka safi na la ushindani walilolionyesha kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Leo hii Ligi ya Tanzania imeingia midomoni mwa watu kwa sababu ya mafanikio ya klabu zetu, hii itaongeza ushawishi kwa wachezaji wa nje ya Tanzania kutamani kuja kucheza ligi ya hapa nchini hususani kwenye klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam.

Uwezo na ushindani waliouonyesha Yanga kwenye michuano hii umemfanya Rais wa nchi yetu, Samia Suluhu kuwapa mwaliko wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa kupata nao chakula cha mchana kwa lengo la kuwapongeza.

Rais Samia ameona jitihada za klabu hii katika kulitangaza taifa kwenye mashindano ya kimataifa, mafanikio ya Yanga ni mafanikio ya nchi kwenye soka, sasa Afrika inafahamu uwezo wa klabu zetu kwenye mashindano ya kimataifa.

Hakuna ubishi Yanga wanastahili pongezi kwa kile walichokifanya msimu huu kwenye michuano ya kimataifa, kupata ushindi mbele ya wenyeji hasa klabu za Afrika Magharibi sio jambo dogo hata kidogo.

Miaka ya nyuma tulizoea kuona klabu zetu zikienda nje ya nchi zinafuata vipigo na pengine matokeo ya kudhalilisha, lakini kwa sasa mambo yamekuwa tofauti, klabu za Tanzania zinaweza zikapata matokeo ugenini.

Kile walichokifanya Yanga kinapaswa kuigwa na klabu zingine za Tanzania hususani zile zitakazopata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.

Yanga na Simba tayari zimejihakikishia kucheza michuano ya kimataifa mwakani, lakini Azam na Singida Big Stars nazo zimeshatanguliza mguu mmoja kushiriki mashindano ya kimataifa, kile walichokifanya Yanga wanapaswa kukiiga.

Hakuna ubaya kuiga mafanikio ya mpinzani wako, Simba, Azam na Singida ziige kile ambacho Yanga wamekifanya msimu huu, zijiandae na zijipange kufanya vizuri, hakuna kinachoshindikana kwenye soka unapokuwa na nia na malengo.

Nipashe tunaipongeza Yanga kwa mafanikio waliyofikia msimu huu, wamejitangaza, wameitangaza ligi yetu lakini zaidi wameitangaza nchi kwenye medali za soka, wanastahili pongezi za taifa kwa kile walichokifanya, hongera Yanga, hongera wachezaji, viongozi na mashabiki wake.