Hivi karibuni ilibainika katika Mkoa wa Mbeya kuwapo watu wanaoiba vibao hivyo ambavyo vimewekwa ili kutambulisha mitaa na kurahisisha wageni kufika mitaa husika kwa urahisi.
Katika kudhibiti wizi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, ameagiza watendaji wa kata, vijiji na maofisa tarafa kufanya msako na kuwakamata wananchi wote wanaohusika kuiba vibao hivyo vya anwani za makazi vilivyowekwa kwenye mitaa mbalimbali mkoani humo.
Agizo hilo alilitoa wakati alipopokea ripoti ya uchambuzi ya Sensa ya Watu na Makazi kwa mkoa wake ambayo ilihusisha viongozi mbalimbali wa mkoa huo na timu ya wataalam waliohusika kwenye mchakato wa kukamilisha kazi hiyo.
Alibaini kuwapo kwa baadhi ya maeneo vibao kung’olewa na watu wasiokuwa waadilifu na kwenda kuviuza kama vyuma chakavu na wengine kuweka katika ofisi zao.
“Tayari watu wameanza kung’oa vibao kwenye mitaa yao na kwenda kuviuza kama vyuma chakavu ili wajipatie pesa sasa naagiza watendaji wote na maofisa tarafa kushughulikia suala hili, najua mnawafahamu na mtawakamata nendeni mkalitekeleze hili ili liwe fundisho kwa wengine kwa sababu wanatuhujumu.”
Kwa kweli kitendo hicho kinasikitisha na kinakwamisha jitihada za serikali za kurahisisha mawasiliano kwa kuwa kuondolewa kwa vibao hivyo kutasababisha wageni kushindwa kufika maeneo wanayokusudia.
Katika miji mingi kwenye nchi zilizoendelea na baadhi ya zinazoendelea, imekuwa rahisi kwa mgeni anapoelekezwa kufika kwa urahisi kutokana na kuwapo kwa anwani za makazi na vibao vinavyoongoza kwenye mitaa hiyo.
Wageni kutoka nchi za mbali wanapotembelea nchi za kigeni hupata urahisi wa kufika mahali wanapokwenda kutokana na kuwapo na mipango miji mizuri na yenye anwani za makazi.
Mgeni anaweza kufika sehemu husika kwa kuangalia tu ramani, bila kumuuliza mtu yeyote kumuelekeza.
Serikali inajitahidi kuifanya nchi kuwa kwenye mipango miji mizuri kwa kuweka anwani za makazi ili kuwarahisishia wageni.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa Mkoa wa Mbeya, idadi ya watu ni 2,343,754 ikilinganishwa na mwaka 2012 iliyokuwa 1,708,548 sawa na ongezeko la 635,206.
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 3.2 ambayo sasa mkoa utaweka mipango madhubuti kwa ajili ya kukamilisha shughuli za miradi ya maendeleo.
Takwimu hizo zitasaidia kuongeza uwazi ili wawe na uelewa wa matumizi ya matokeo ya sensa kwa ajili ya kutoa michango yao kwa ajili ya maendeleo ya taifa na kushauri namna bora ya kuyapima.
Mstahiki Meya wa Halmshauri ya Jiji la Mbeya, amehakikisha jiji hilo kuandaa mipango kabambe kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kwa kuzingatia idadi ya watu.
Pia, wananchi wameombwa kuishauri serikali namna bora ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kusisitiza kutoa ushirikiano ili ikamilike kwa wakati.
Katika hili wananchi lazima wakumbuke kuwa maendeleo yoyote yanayofanywa ni kwa ajili yao, kuhujumu maendeleo hayo ni sasa na kujihujumu wenyewe.