Wilayani Kahama ni kawaida kusikia taarifa za uzazi miongoni mwa watoto na kwa mwaka jana pekee mabinti 2,619 walijifungua, anaeleza Mratibu wa Mama na Mtoto wa Halmashauri ya Kahama Caroline Maliseli.
Aidha, kujifungua katika umri mdogo ni kuhatarisha usalama wa mjamzito na mtoto wake tumboni kwa sababu nyonga zinakuwa hazijafunguka, kadhalika wengi hawana uelewa juu ya kuhudhuria kliniki ili kujua maendeleo ya mtoto na kujifungulia nyumbani na kuzalishwa na watu wasiokuwa na utalaamu, anaonya mratibu huyo.
Anasema wimbi la wasichana wadogo kujifungua kabla ya wakati wao limekuwa kubwa na mwaka jana pekee jumla ya wasichana 2,619 walijifungua chini ya umri huo sawa na asilimia 16.
Anasema, mwaka huo wajawazito 17,605 walijifungua kati ya hao 2,619 walikuwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 na wengi wao ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na tatizo la ndoa za utoto ni kubwa na linapaswa kutafutiwa ufumbuzi.
Aidha, anasema, hao ni baadhi ya wanaofika katika vituo vya afya na kupata huduma, huku kundi kubwa likijifungulia majumbani na kufikia 497 sawa asilimia tatu na kuzalishwa na watu wasiokuwa wataalamu wa afya wakiwemo mama wakwe, waganga na wakunga wa jadi wote wakihatarisha maisha ya mama na mwana.
“Rika hili wakati wa kujifungua wanatumia pia dawa za kuongeza uchungu zinazowasababishia mfuko wa uzazi kupasuka na mtoto kunywa maji na kupoteza maisha, ofisini kuna chupa nyingi za dawa hizo na yote hayo wanayafanya kwa maelekezo ya mama wakwe. ,”anasema Caroline
MATUKIO YA VIFO;
Anaeleza kuwa mwaka 2021 mjamzito alizalishwa ndani ya duka la dawa na mhudumu katika Halmashauri ya Msalala, ambaye alitumia mbinu zilizosababisha mtoto kukatika kichwa, baada ya tukio hilo alitoweka na mama akabaki anatokwa na damu nyingi.
Caroline anasema mzazi alifikishwa hospitalini na kufanyiwa upasuaji kuondoa kichwa cha mtoto tumboni ambacho kilikuwa kikubwa na kwamba alikuwa hahudhurii kliniki kipindi cha ujauzito, licha ya kunusurika, alimpoteza mtoto.
Anawaonya kinamama kuacha tabia za kukwepa kliniki badala yake wanapopata uchungu wafike vituo vya afya na pia kuachana na tiba za asili ambazo ni hatari.
Kadhalika anasema,mwingine alikuwa mkazi wa kata ya Mhungula Manispaa ya Kahama alikuwa akizalishwa na mama mkwe wake baada ya kupata uchungu na mtoto alitanguliza miguu na walipomvuta walimkata kichwa pia, walimsaidia mama kwa kumfanyia upasuaji na kuondoa kichwa, na wote wanaozalishwa kwa njia za kienyeji wanapoteza vichanga vyao.
Anasema, pia katika kata ya Isagehe mjamzito mwenye umri chini ya mika 18 alipelekwa kwa mganga wa jadi na mama yake mzazi kuzalishwa kienyeji kwa kutumia vitu mbalimbali vilivyosababisha mtoto kubonyezwa fuvu la kichwa.
Walimfikisha hospitalini na kumsaidia hadi akajifungua salama lakini maumbile ya mzazi yalivimba kutokana na kuchokonolewa na vitu ambavyo si salama, anaeleza Caroline.
MAONI WANAJAMII
Joseph Masanja, mwanafunzi wa kidato cha tatu Sekondari ya Nyikoboko anasema, kuna mwanafunzi mwenzao alipata ujauzito wakiwa kidato cha pili aliacha masomo hata kabla ya kufanya mtihani wa kuingia kidato cha tatu na alijifungua kwa njia ya upasuaji, mtoto yupo salama lakini mama yake alipata maradhi ambayo hakuyataja.
Katika Shule ya Msingi Shilela, Salumu Mashaka wa darasa la sita anasema, jirani yake alifaulu kujiunga na Sekondari ya Mwalimu Nyerere iliyopo Halmashauri ya Msalala, wazazi wake waligoma kumsomesha wakidai hawana fedha kumbe walitaka kumwozesha lakini walitoa taarifa polisi na mpango wao ukatibuliwa na sasa anaendelea na masomo.
Mkazi wa kata ya Kilago-Kahama Raphael Mazigwa, anasema,ili kukomesha ukatili kwa watoto hususani kuwaozesha kwa tamaa ya mali, ilihali wanahitaji kusoma ni vema jamii ikawa inaelezwa hatua zinazochukuliwa kwa wale wanaobainika kutenda vitendo hivyo ili ijue adhabu ambazo zimekuwa zikitolewa kwa watuhumiwa.
Aidha, anawashauri watendaji wa mitaa na kata kutojihusisha katika vitendo vya upatanishi pale mtoto au mwanafunzi anapopata ujauzito kwani wanamuachia majeraha moyoni mhanga hivyo wahakikishe mashauri wanayoyapata ofisni mwao wanayafikisha katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
USTAWI WA JAMII.
Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Swaiba Chemchem, anasema, ukatili wa kijinsia kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 bado upo na unatakiwa kudhibitiwa ili kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto zao za kielimu.
Anasema, watoto 881 wamefanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili na unyanyasaji kwa kipindi chama miezi tisa mfululizo mwaka jana.
Aidha, anasema, kati ya hao 255 walikuwa wa kiume na 469 wa kike na vitendo hivyo vimekuwa vinafanywa na watu wanaoishi nao na kuwaamini tena wanaojua kuwa ni kosa kisheria na wanapobainika wamekuwa wakishtakiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 20019.
Swaiba anasema, kati ya hao ndoa za utotoni zilikuwa 11, mimba za utotoni 31 kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kutupa watoto matukio saba, ajira za utotoni 14 na usafirishaji haramu wa watu kutoka sehemu moja hadi nyingine ilikuwa mikasa 101 na kuwaomba wazazi na walezi kushirikiana pamoja kutokomeza vitendo hivyo.
“Utoaji wa elimu ya ukatili na madhara yake kwa kushirikiana na mashirika ya kiraia yanayofanya kazi na serikali ikiwemo SHDEPHA+ imewaibua wananchi kujitokeza na kutoa taarifa na kuwanusuru watoto wanaozeshwa wakiwa bado shuleni, na bado tunaendelea kuchukua hatua pale tunapobaini wazazi kuhusika moja kwa moja,”anasema Swaiba.
UBAKAJI WAONGEZEKA
Mwenyekiti wa Asasi ya Wanawake 100,000 mkoani Shinyanga, Anascholastica Ndagiwe, anasema, wanafunzi au wasichana wanaopata ujauzito wengi wanabakwa na hivi karibuni alibakwa mwanafunzi wa darasa la nne na mshitakiwa kuhukumiwa miaka 35 jela licha ya hukumu kutolewa akiwa nje kwa dhamana, na hata sasa hajulikani alipo.
Anasema pia baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa chanzo cha watoto wao kupata ujauzito wakiwa shuleni na familia nyingi wanatelekeza watoto na mabinti wakilazimika kuwalea wadogo zao na hii inasababisha kuingia kwenye ngono wakiwa na umri mdogo ili kupata fedha za kujikimu.
John Banda, Mwalimu wa Taalumu wa Sekondari ya Nyikoboko anakiri kuwepo kwa tatizo la wanafunzi wa kike kupata ujauzitio na kushindwa kuendelea na masomo na kwamba wanakuwa na uwezo mkubwa darasani na mwaka 2022 kuliripotiwa kesi moja ya mwanafunzi wa kidato cha tatu kupata ujauzito.
Halikadhalika anasema, kuna mwanafunzi alifanya mtihani akiwa na ujauzito bila wao kujua na alifaulu kuingia kidato cha tatu lakini alishindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya mimba na vitendo hivyo vya kikatili vinafanyika ndani ya jamii wanazotoka na baadhi ya wazazi na walezi ni watuhumiwa moja kwa moja.
Joseph Samwel kutoka kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Shilela wilayani Kahama anasema, kila mwezi wamekuwa na utaratibu wa kutembelea kijiji kimoja na kutoa elimu ya madhara ya ndoa na mimba za utotoni na zile wanazozibaini wanaziripoti katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.









