Tunaipongeza serikali utekelezaji mradi wa Bwawa la Julius Nyerere

27Feb 2024
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tunaipongeza serikali utekelezaji mradi wa Bwawa la Julius Nyerere

HATIMAYE serikali imeingiza megawatt 235 kwenye Gridi ya Taifa ambazo zimepunguza mgawo wa umeme kwa asilimia 85, baada ya kuwasha mtambo namba tisa kati ya idadi hiyo inayowezeshwa jumla ya megawatt 2,115 katika Bwawa la Nyerere.

Ni hatua iliyotangazwa juzi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, ambaye pia aliahidi kuwa mwezi ujao Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Misri, Abdel-Fatah Alsisi, watazindua mtambo namba nane na hivyo kuwezesha nchi kuwa na megawatt 470 zinazoongezwa kwenye Gridi ya Taifa kutoka mradi wa kufua umeme wa maji wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).

 

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu Biteko, kuwashwa kwa mtambo huo kumefanya upatikanaji umeme nchini kuwa wa asilimia 98, mgawo umepungua na utakwisha mwezi ujao.

 

Nipashe tunapongeza hatua hiyo ya serikali ambayo si tu kwamba inakwenda kutatua kero ya muda mrefu ya mgawo wa umeme nchini, bali pia inaingiza nchi kwenye historia ya utekelezaji wa mradi mkubwa.

 

Mradi huo wenye thamani ya Sh. trilioni 6.6, ulianza kutekelezwa mwaka 2015 licha ya kuwapo ukosoaji mkubwa ndani ya nje ya mipaka ya Tanzania, uliojikita katika hoja ya athari za kimazingira. Serikali chini ya uongozi wa Rais John Magufuli ilisisitiza kupuuza ukosoaji huo.

 

Tunapongeza uthubutu huo wa serikali ambao sasa unakwenda kuifanya nchi kuwa na 'utajiri wa umeme'. Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu Biteko, upungufu uliokuwapo ni megawatt 200 hadi 400, hivyo kuwashwa kwa mtambo namba tisa kunafanya nchi kuwa na umeme wa ziada megawatt 70, hata kabla ya kuwasha mitambo mingine minane iliyo katika ujenzi.

 

Serikali inastahili pongezi kwa jitihada zake hizo za kuhakikisha inamaliza kero ya mgawo wa umeme nchini na kuondoa malalamiko miongoni mwa wananchi kwa kukosa nishati ya uhakika.

Pamoja na pongezi hizo, Nipashe tunatambua kwamba mahitaji ya umeme yanaongezeka kila kukicha, hivyo serikali inapaswa kuongeza vyanzo vingine kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana nchini.

 

Nipashe tunatambua kuwa zipo nchi zilizo na vyanzo vya uhakika vya umeme, lakini kikwazo kikubwa kimekuwa wizi wa umeme unaofanywa na watu wake, maarufu vishoka.

 

Hivyo, serikali inapaswa kulinda miundombinu ya umeme ili isihujumiwe na watu wachache kwa manufaa yao binafsi na kuhakikisha hakuna wizi wa umeme, ikizingatiwa mradi huo wa Bwawa la Nyerere umetumia fedha nyingi.

 

Shirika la Umeme (TANESCO) linafanye ukaguzi wa mara kwa mara katika miundombinu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha hakufanyiki vitendo vya udanganyifu katika huduma ya umeme kwa wananchi.

 

Pia elimu itolewe kwa wananchi ili washiriki kulinda miundombinu ya umeme na madhara yanayowezesha kusababishwa na vitendo hivyo.

 

Tunaipongeza serikali kwa utekelezaji mradi wa Bwawa la Nyerere.