Kuna jambo la kujifunza kutoka mradi Bwawa la Julius Nyerere 

01Mar 2024
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kuna jambo la kujifunza kutoka mradi Bwawa la Julius Nyerere 

FEBRUARI 25, mwaka huu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alifanya ziara katika mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere, kwa lengo la kukagua maendeleo ya kazi hiyo.

Ziara hiyo ilijumuisha maofisa waandamizi wa wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu, mhandisi Fulcheshmi Mramba, watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Boniface Nyamo-Hanga, viongozi wa mkoa wa Pwani wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge, wakuu wa vyombo vya habari, wahariri na waandishi wa habari.

Katika ziara hiyo ambayo pia ilimjumuisha Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ilishuhudiwa mtambo mmoja kati ya tisa ya kuzalisha umeme katika bwawa hilo, wenye megawati 235 ukiwa umewashwa, hivyo kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa.

Hatua hiyo imesaidia kupunguza makali ya mgawo wa umeme yaliyokuwa yakiwakabili wananchi kwa miezi kadhaa. Licha ya kuingizwa kwa kiwango hicho, pia ilishuhudiwa mtambo mwingine ukiwa katika hatua za mwisho za kukamilika, hali itakayowezesha kuingizwa megawati zingine 235 na kuingizwa kwenye gridi na hatimaye tatizo la mgawo au kukatikakatika kwa umeme kuwa historia.

Hiyo ni habari njema kwa kuwa kuwapo nishati hiyo kwa wingi, kutachochea maendeleo ya uchumi katika sekta za uzalishaji na uboreshaji huduma katika miradi ya kijamii kama vile afya, elimu na maji kwa kuwa umeme ni nyenzo muhimu katika kufanikisha azma ya jambo lolote.

Pamoja na furaha inayotokana na kuongezeka kwa umeme katika gridi ya taifa, liko jambo moja ambalo linatoa funzo kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo ile ya kimkakati. Jambo hilo ni ushirikishaji wa wazawa katika huduma mbalimbali kupitia miradi hiyo, maarufu kama ‘local content’. 

Katika mradi huo, huduma mbalimbali kama vile ununuzi wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa bwawa hilo, sare, vyakula na viburudisho wa watumishi na wageni, vilitolewa na kampuni za ndani.

Akijibu moja ya maswali yaliyoulizwa wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Mramba alisema suala hilo lilizingatiwa kikamilifu kwa kuwawezesha Watanzania wanaozalisha vifaa vinavyohitajika katika mradi huo pamoja na huduma mbalimbali kupewa kipaumbele. Mhandisi Mramba alibainisha kwamba vifaa kama mabati, saruji na nondo zilizotumika kwenye mradi zilinunuliwa kutoka kwenye viwanda vya ndani.

Alisisitiza kwamba Watanzania walipewa kipaumbele katika utoaji wa huduma mbalimbali kutokana na mahitaji yaliyokuwapo na yaliyopo katika mradi huo unaoendelea kutekelezwa. Pia alisema hata mshauri mwelekezi, alitoka ndani ambaye ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia kitengo chake cha ushauri elekezi (TECU). Hata vyakula vinavyotolewa kwenye mradi huo kama vile unga, mchele, samaki na nyama, ni dhahiri vinatolewa na wazabuni wazawa kama ilivyoonekana.   

Inatia faraja kuonyesha kwamba wazawa wamepewa kipaumbeke katika utoaji wa huduma kupitia mradi huo, hivyo kunufaika kiuchumi na kijamii, vinginevyo huduma hizo zingetolewa na kampuni za nje hatimaye Watanzania kuachwa kama washangiliaji wa mchezo.

Kutokana na ushirikishwaji huo wa Watanzania  katika utoaji wa huduma mbalimbali ikiwamo viwanda vya ndani kupewa nafasi ya kuuza vifaa vyao, ni hatua kubwa kimaendeleo. Kwa kufanya hivyo, wananufaika moja kwa moja kwa kupata zabuni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi.

Miaka ya nyuma iliwahi kuelezwa kuwa baadhi ya huduma vikiwamo vyakula zilikuwa zikitolewa na kampuni kutoka nje hali ambayo iliwanyima Watanzania fursa licha ya kuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo.

Hivi sasa kuna miradi mbalimbali inayoendelea kama vile ujenzi wa barabara na reli ya kisasa kwenye maeneo mbalimbali, hivyo wahusika katika utekelezaji wa kazi hizo, hawana budi kujifunza kupitia mradi wa Bwawa la Julius Nyerere.