Kitendo hicho kilisababisha taharuki kubwa na baadhi ya wateja wao kukosa haki yao ya kupata taarifa kupitia magazeti yanayouzwa na wafanyabiashara hao.
Katika taarifa hiyo ya TEF ilibainisha kuwa Oktoba, mwaka jana, serikali ilianza kuwaondoa wafanyabiashara wadogo pembezoni mwa barabara za jiji la Dar es Salaam, lakini wauzaji magazeti hawakuondolewa kutokana na sababu za msingi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014, nyongeza ya 9(3) inatambua magazeti kuwa nyenzo ya elimu sio biashara.
Sheria hiyo inafanana na sheria zote za kodi na mapato na VAT duniani kote na ndiyo maana katika miji yote kuna meza za magazeti na vitabu katika kona za mitaa kwa ajili ya kuendeleza elimu na maarifa kwa watu wake.
Tunatambua kuwa uondoaji wa wafanyabiashara waliokuwa wametanda katika kila kona za barabara Jiji la Dar es Salaam, umesaidia kwa kiasi kubwa kupunguza msongamo uliosababisha hata wanaotembea kwa miguu kushindwa kupita kwenye njia walizotengewa.
Pia, baadhi ya wafanyabiashara walidiriki kugeuza vibanda vilivyojengwa kwenye vituo vya mabasi kwa ajili ya kuwakinga na jua, mvua wasafiri, kuwa vya kufanyia biashara ndogo ndogo na wengine kudiriki kuweka majiko ya kupikia ambayo yangeweza kusababisha hatari kwa vyombo vya moto.
Hata hivyo, jiji liliruhusu wafanyabiashara wa magazeti kuendelea kuweka meza zao ili kuwapa wateja wao haki ya kupata habari na taarifa.
Lakini, tukio la juzi la wafanyabiashara hao kutimuliwa na askari wa jiji lilisababisha sintofahamu na vyombo vya habari vinavyotegemea mauzo yanayotokana kwenye magazeti hayo kwa ajili ya kujiendesha kuingia hasara kwa bidhaa hiyo kurudi kwa wingi bila kuuzwa.
Tunajua katika kutafuta maelewano ni lazima busara ichukue nafasi yake na popote kwenye maelewano hakuna kinacho haribika.
Hivyo ni busara ikatumika elimu kuwaelimisha wafanyabiashara hao kabla ya kuchukua hatua iliyofanywa na askari hao wa jiji na kusababisha kilichojitokeza.
Jana, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ilitoa taarifa ya ufafanuzi kuhusu tukio lililotokea juzi dhidi ya wafanyabiashara hao wa magazeti ikieleza kuwa, wafanyabiashara hao waliondolewa kutokana na kuuza bidhaa nyingine zaidi ya magazeti.
Taarifa hiyo ilisema kuwa wafanyabiashara hao wanaruhusiwa kuendelea kuuza magazeti kwa kuzingatia maelekezo ya kufanya biashara ya magazeti pekee.
Tunasema taarifa hiyo ingetolewa kabla ya kuchukua hatua iliyochukuliwa ingesaidia kuondoa mtafaruku huo. Na elimu ni kitu cha msingi kwa wafanyabiashara kuelewa nini cha kufanya na nini kinatakiwa kisifanyike wanapofanya shughuli zao.