Dosari hii irekebishwe masoko yawe na faida

23Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Dosari hii irekebishwe masoko yawe na faida

KARIBU kila mkoa Tanzania Bara sasa kunashuhudiwa kumejengwa au kunajengwa masoko na vituo vya kisasa vya mabasi, ujenzi huo ukigharimu mabilioni ya shilingi.

Hata hivyo, kinyume cha matarajio ya wengi kwamba masoko na vituo hivyo vingelikuwa na manufaa kwa Taifa kiuchumi, imebainika kwa sasa kwenye baadhi ya mikoa, hakuna faida inayopatikana kutokana na uwekezaji huo.

Mathalani, katika ukaguzi wa kitaalamu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambao ripoti yake inafanyiwa kazi na Bunge kwa sasa, imebainika masoko na vituo vya mabasi havijawa na matokeo chanya kimapato.

CAG katika ukaguzi wa ufanisi kwenye usimamizi wa masoko na vituo vya mabasi nchini, ameweka bayana kwamba ameshindwa kuiona faida ya uwekezaji huo wa zaidi ya Sh. bilioni 530 kwenye miradi hiyo.

Kimsingi, kanuni za uanzishaji wa serikali za mitaa zinatamka bayana kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zina jukumu la kudhibiti na kusimamia masoko na vituo vyote vya mabasi.

Hata hivyo, kilichobainika kuwa nyuma ya kutoonekana faida kwenye uwekezaji huo, ni usimamizi mbovu wa masoko na vituo vya mabasi unaochagizwa na: Kukosekana kwa umakini wakati wa kufanya upembuzi yakinifu; mazingira yasiyoridhisha ya utendaji kazi; ukosefu wa ofisi za wasimamizi wa masoko na kutokuwapo kwa mikataba ya upangaji.

Vilevile, zipo dosari zingine zinazojumuisha migogoro ya ardhi iliyochangiwa na ukosefu wa hatimiliki na kuwapo kwa viongozi wa umma ambao hawafanyi kazi kwa manufaa ya umma, hivyo kuchangia usimamizi hafifu katika uendeshaji wa masoko na vituo vya mabasi.

Nipashe tunaona kuna haja kumulika vikwazo tajwa ili masoko na vituo vya mabasi viwe na tija ikizingatiwa kwamba uwekezaji katika miradi hiyo umegharimu zaidi Sh. bilioni 530, ambazo ni mali ya umma, huku baadhi ya miradi ikibainika haitumiki kikamilifu.

Ripoti ya CAG inabainisha masoko na vituo vya mabasi vyenye dosari hizo, likiwamo Soko la Chuno katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani lililojengwa chini ya mradi wa Miji ya Kimkakati Tanzania kwa gharama ya Sh. bilioni 5.54 huku makadirio ya makusanyo yake kwa mwaka yakiwa Sh. milioni 138.1.

Inashtusha pale inapobainika soko hilo lina vibanda 237 vilivyo wazi kwa zaidi ya miezi minne na kusababisha hasara ya mapato ya Sh. milioni 32 huku masoko ya Skoya na Chiyangu pamoja na Kituo cha Mabasi cha Chipuputa katika Manispaa hiyohiyo ya Mtwara-Mikindani yakiwa wazi kwa kipindi cha mwaka mzima na kusababisha hasara ya jumla Sh. milioni 131.

Kwa kuzingatia uzito wa suala hili, Nipashe tunaona kwamba suala la kutotumika kwa masoko na vituo vya mabasi vilivyojengwa lisiposhughulikiwa ipasavyo na kwa wakati, linaweza kuchelewesha kupatikana kwa faida itokanayo na uwekezaji mkubwa uliofanywa.

Ni rai yetu kwa mamlaka husika kuchukua hatua kwa kuwa kutotumika kwa miundombinu hii kutasababisha uchakavu na hivyo kushusha thamani yake.

Hivyo, tunaishauri serikali kupitia menejimenti za Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuimarisha usimamizi wa mfumo wa masoko na vituo vya mabasi kwa kuhakikisha wafanyabiashara wote wanatumia masoko na vituo vya mabasi vilivyojengwa badala ya kutumia maeneo yasiyo rasmi ili kupata thamani ya fedha za miundombinu iliyojengwa.

Kuepuka hasara tajwa, Nipashe pia tunaona kuna haja serikali ihakikishe upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kama vile umeme, maji, idadi ya watu, makazi na mengine yanayofanana na hayo, uzingatiwe wakati wa upembuzi yakinifu kwa kuwa kuwapo kwake kunatengeneza mazingira mazuri ya kuvutia biashara.