Mpango wa kutambua wabunifu uwe chachu ya kuibua wengi zaidi

22Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mpango wa kutambua wabunifu uwe chachu ya kuibua wengi zaidi

SERIKALI imeanza utaratibu wa kuwatambua wabunifu nchini kupitia mashindano kutokana na kuwapo kwa mwongozo wa kutambua na kuendeleza ubunifu na maarifa asilia.

Katika mwongozo huo wabunifu 2,647 wametambuliwa na kuibuliwa katika mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu) ndani ya miaka minne tangu mwaka 2018.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwasasa inafanya mapitio ya rasimu ya mwongozo huo ili kukidhi mahitaji yaliyoko kwa kuibua wabunifu wengi zaidi na kuwaendeleza.

Imeelezwa kuwa bila kuwapo na sayansi, teknolojia na ubunifu, maendeleo yanayotamaniwa nchini ni ngumu kuyafikia.
Nchi nyingi duniani zinaendelea kutokana na kujikita katika sekta ya sayansi na teknolojia ndivyo dunia inavyokwenda kwa sasa.

Imeshauriwa mapitio ya mwongozo huo yalenge kuwapo kwa hamasa ili wabunifu waonyeshe ubunifu wao.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wabunifu kutothaminiwa kazi zao au kupata ushirikiano ili kuziendeleza, hali inayowakatisha tamaa.

Kupitia mwongozo huo tuna imani kuwa watu wengi wenye vipaji vya ubunifu watapata fursa ya kuonyesha kazi zao na hatimaye kufikia malengo waliyojiwekea.

Kati ya wabunifu hao waliotambuliwa imeelezwa kati yao 283 wameendelezwa na wapo kwenye hatua mbalimbali huku zaidi ya 26 bunifu zao zikifikia hatua ya kutangazwa kibiashara.

Vikwazo kadhaa vinavyosababisha kutokuwa na wabunifu wengi vimeelezwa kuwa ni suala la mtazamo na uelewa wa masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Pia, kazi zinazobuniwa zinatakiwa kuwa na hatimiliki ili kulinda haki ya mtu isiibiwe na hilo linahitaji elimu ya kutosha kwa wabunifu wetu.

Baadhi ya watu wanaokwamisha wabunifu kusonga mbele ni wanaotoa vikwazo zikiwamo leseni, wakati mbunifu akiwa ndiyo kwanza ameanza kazi hiyo.

Ubunifu ni suala linalomfanya mtu kutumia akili na maarifa ili kitu atakachokibuni kiweze kukubalika mbele ya watu wengine na kuleta tija.

Tunasema hatua inayochukuliwa na serikali kupitia Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara hiyo, Prof. Maulilio Kipanyula, ya kuboresha mwongozo huo ili kuongeza hamasa, kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu hasa kwa ngazi za chini ni wa busara, unatia moyo.

Kwa mujibu wa serikali rasimu ya mapendekezo ya mwongozo huo itajadiliwa na kikosi kazi na kutoa maoni ili kukamilisha mapitio ya mwongozo huo.

Dhamira ya serikali kupitia wizara hiyo ni kuhakikisha mwongozo unaboreshwa ili kukidhi mahitaji ya sasa kutokana na mwongozo wa awali kuwa na upungufu ikiwamo kutoonesha majukumu ya wadau katika kuibua, kutambua na kuendeleza wabunifu.

Ni muhimu kwa vijana ambao kila kukicha wanalia kukosekana kwa ajira wakatumia fursa hii kubuni vitu vitakavyowawezesha kujiajiri.

Mwongozo huo unatoa fursa ya bunifu zitakazoibuliwa kutangazwa kibiashara ili kuleta tija kwa wabunifu hao.
Ni vyema suala hilo likatolewa elimu ya kutosha ili kulinda wabunifu wetu na kuweza kufanyakazi vizuri zaidi.