Mojawapo ni wizi wa mali za maiti wa ajali za barabarani na hata kuwaua majeruhi ili kuwapora mali zikiwamo fedha, vitu vya thamani na mizigo yao.
Uovu huo umekuwa na athari kama majeruhi ambao wangenusurika hospitalini kupoteza maisha baada ya kumaliziwa (kuuliwa) na waporaji.
Lakini, majeruhi kukosa msaada kwa vile badala ya kuokoa maisha ya watu kwanza, wanaofika eneo la tukio wanaanza kupora na kukimbilia vitu ili kuiba mali nyingi lakini si kuokoa binadamu wenzao wanaohitaji msaada.
Athari nyingine ni miili ya ajali kutokutambuliwa hospitalini na kuzikwa na serikali, yote hayo ni kwa sababu vitambulisho vyao vimeporwa na pengine jamaa zao hawakuwa na taarifa za shughuli za ndugu hao iwapo walisafiri.
Ni fedheha kwa taifa pale gari linapopata ajali watu wanaanza kuwaweka majeruhi na marehemu pembeni na kuwapekuwa. Wanawaibia simu, pochi, waleti, saa, mavazi ya thamani, mikanda, mizigo yao na pale inapoonekana majeruhi analeta upinzani anaumizwa zaidi hata kuuawa.
Uporaji hauishii hapo kuna madai kuwa gari nalo huchokonolewa zikaibiwa betri, taa, redio na vifaa muhimu na kama ni usiku hata injini na matairi vinaweza kuibwa.
Wizi wa kupora wafu na majeruhi tena kuwaua ni tabia inayokomaa, kama taifa kinachosikitisha ni kukosekana sauti za mara kwa mara za kutaka kuwe na sheria ya kuharamisha kuibia marehemu wa ajali zozote na majeruhi.
Tunaona kuwa ni wakati wa wadau na serikali kuangalia namna bora ya kudhibiti uovu huu kwa kutunga sheria.
Lakini, tungependa kuona watuhumiwa wa makosa hayo wakifikishwa mahakamani na kuadhibiwa kikamilifu ili kudhibiti mienendo hiyo inayokatisha kinyama maisha ya binadamu hasa wasafiri.
Inashangaza kusikia wapo Watanzania wenzetu wanaokaa kwenye vyumba vya kuhifadhi miili hospitalini kwa muda mrefu bila kutambuliwa na kuzikwa na jamaa zao, badala yake wanazikwa na mamlaka za manispaa na halmashauri za miji na majiji.
Tunajiuliza hivi kuna watu ambao hawana ndugu? Japo inatokea miili haikutambulika kisa haikuwa na vitambulisho, lakini hili ni jambo lisilokubalika.
Tunaoimba serikali ijitahidi kuweka kamera za kurekodi matukio za CCTV kwenye barabara kuu zote kuanzia Dar es Salaam hadi mikoani zinapoishia.
Ni vyema pia halmashauri za majiji, miji na manispaa mikoani na wilayani nazo zikaweka CCTV kamera kurekodi hali ya usalama barabarani na kudhibiti uhalifu ukiwamo kuwaibia majeruhi, kuwaua na kuwapora wafu badala ya kusaidia na kuokoa maisha yao.
Wadau wasikae kimya wakiwamo asasi za kiraia za kutetea wasafiri, usalama wa abiria na Jeshi la Polisi wakati wa kampeni ya Wiki ya Usalama Barabarani, isiishe kukagua magari wawe wabunifu na kuzungumzia haki ya abiria aliyepata ajali.
Wawakumbushe vijana na kuhamasisha kuhusu usalama ukiwamo haki ya maisha ya majeruhi wa ajali za barabarani na ulinzi wa mali zao.
Inavyoelekea mazoea ya kuibia majeruhi yamekuwa na sasa ni jambo linalokubalika kama wanavyofaniwa wezi mitaani.
Inaelekea kuwa ni jambo la kawaida mwizi kuteswa, kupigwa na kuchomwa moto.
Hivi mienendo hiyo ni sahihi? Kwanini tabia hizo ziendelee miaka na miaka za kuua watu kisa kelele za mwizi na kumfukuza wanayemuona mbele yao bila kuwa na uhakika.
Tunashauri mambo hayo yaanze kukemewa na kukomeshwa si jambo jema kuuana si vibaka, majeruhi wa ajali barabarani wala kuiba mali za wasafiri baada ya vyombo vya moto kupinduka.