Wachezaji epukeni usajili unaofaidisha timu pekee

25Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wachezaji epukeni usajili unaofaidisha timu pekee

LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/ 2022 inatarajia kufikia tamati Juni 29, mwaka huu kwa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo kushuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu.

Hata hivyo wakati ligi hiyo ikielekea ukingoni tayari bingwa mpya ameshapatikana naye si mwingine ni klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam.

Yanga iliwavua mabingwa mara nne mfululizo, Simba wiki iliyopita baada ya kufikisha pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine, hapo ilikuwa na mechi tatu mkononi.

Kwa heshima ya kutwaa taji hilo, Yanga inayofundishwa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, itakabidhiwa kombe lake leo kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya baada ya kumalizika kwa mechi ya raundi ya 29 dhidi ya wenyeji Mbeya City.

Hii inamaanisha kwamba vita iliyobakia katika mechi za hatua ya lala salama ni ya kusaka tiketi mbili za kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), zilizobakia baada ya Simba iliyoko kwenye nafasi ya pili tayari kupata nafasi hiyo kutokana na pointi zake 60 ilizonazo.

Vita hiyo inaweza tu isiwe na kusaka tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini ikawa ni kusaka zawadi ya fedha zitakazotolewa na wadhamini wa ligi hiyo, Kampuni ya Azam Media ambao msimu huu watatoa bonus hadi kwa timu itakayoshuka daraja.

Kwa kifupi, vita iliyopo au michezo ambayo itakuwa na ushindani au inayotakiwa kuangaliwa kwa jicho la tatu ili kuepuka upangaji matokeo ni ile inayohusisha timu zilizoko kwenye janga la kushuka daraja.

Kumalizika kwa msimu huu ndio ishara sahihi ya kuanza kwa maandalizi ya msimu mpya wa 2022/2023.

Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo liko chini ya Rais, Wallace Karia na Katibu Mkuu, Wilfred Kidao, limeshatangaza dirisha la usajili litafunguliwa rasmi ifikapo Julai Mosi na kufungwa Agosti 31, mwaka huu.

Lakini pia likiweka wazi usajili wa dirisha dogo utafanyika kuanzia Desemba 16, mwaka huu hadi Januari 15, mwakani.

Klabu zimetakiwa kutumia muda huo kukamilisha usajili mpya na taratibu za uhamisho kwa nyota wote na ukihusisha timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake.

Kuelekea mchakato huu, wachezaji na timu zimeshaanza kufanya mazungumzo ya kusaini mikataba huku wengine wakiwa tayari wamekamilisha mazungumzo hayo na kuanza kutambulishwa.

Mara nyingi wachezaji ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa mazungumzo hayo kwa kusaini mikataba ambayo inawapa upendeleo klabu na kuwaweka kifungoni wao, hasa pale wanapotaka kuondoka na kujiunga na klabu nyingine ama kwa kupata ofa nono au kujaribu changamoto mpya baada ya kuishi klabu moja kwa muda mrefu.

Umefika wakati wachezaji kupitia mawakala, mameneja, wazazi au walezi wao wanaowasimamia kuwa makini na mikataba inayolenga kuwaumiza wachezaji na hivyo kuonekana kama mikataba ile ya wakoloni ambayo iliwaumiza babu zetu.

Wachezaji mnatakiwa kuhusisha mawakala au wanasheria kabla ya kusaini mikataba ili kujiweka mahali salama na kujiepusha na hatua za kufungua kesi baada ya kubaini klabu iliweka vipengele tata kwenye mkataba ambao ulisaini na hivyo kukuwekea ugumu pale unapopata fursa mpya.

Viongozi wa klabu watendeeni haki wachezaji kwa kuacha tabia ya kuwabana au kuwawekea ngumu vijana wenu hasa pale wanapopata ofa kwa klabu nyingine/ zingine za ndani au nje ya nchi.

TFF pia iendelee kuwasimamia wachezaji hasa wazalendo kwa sababu wanapopata changamoto ya kuachwa au kunyimwa baraka za kujiunga na timu nyingine, vitendo hivyo vinachangia kurudisha nyuma vipaji vyao na hali hiyo kuigharimu nchi kwa kushindwa kuitwa kwenye timu za taifa pale wanapohitajika.

Tunawakumbusha wachezaji pia kuacha kukurupuka kusaini mikataba bila ya kuelewa vipengele lakini pia kutoweka mbele maslahi hali ya kuwa hawana uhakika wa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza katika timu mpya inayowasajili na hivyo kuchangia kuua kipaji chake mwenyewe.