Tuzilinde sanaa zetu zisipoteze uasili wake

27Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuzilinde sanaa zetu zisipoteze uasili wake

KATIKA karne ya 21 teknolojia ya televisheni na maonyesho mbalimbali vimeitangaza sanaa tasnia ya filamu kwa watu wote; watazamaji wa mijini na vijijini katika nchi nyingi zinazoendelea.

Hata hivyo, filamu nyingi zinazosambazwa kimataifa na kupenya soko la nchi nyingi ni zile zinazozalishwa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.

Filamu pia zimekuwa zikitumika kama njia muhimu ya uchumi, hali iliyofanya kuwa nyenzo muhimu itumiwayo na nchi za Ulaya na Amerika.

Mwanzoni mwa miaka ya 1970, dunia ilishuhudia utengenezwaji wa sinema zipatazo 3,500 kila mwaka. Ingawa ni asilimia tano tu ya sinema hizi zilitengenezwa Marekani, lakini filamu za Marekani ndizo zilizochukua asilimia 50 ya muda katika vituo mbalimbali vya televisheni.

Mafanikio ya masoko ya filamu na televisheni ya Marekani kwa kiasi kikubwa yametokana na mkusanyiko wa kampuni za Marekani, Vyama vya Wasanii na kampuni kubwa ambazo zimewekeza fedha nyingi.

Kusambaa kwa wingi kwa filamu za Magharibi katika nchi zinazoendelea inachukuliwa kama hali ya kutiliwa wasiwasi na makundi mengi, kwamba filamu hizo zinaweza kubadilisha hali ya kisiasa na kiuchumi ya nchi zinazoendelea na hata mitazamo ya maisha.

Kama mipango madhubuti haitaweza kufikiwa na serikali zetu, hofu za wengi kuhusu ukandamizaji wa kisiasa zitaongezeka.

Filamu huweza kutoa ujumbe tofauti kwa kila mtazamaji na huweza kushawishi na kutoa taswira ya kipekee kwa kila mtu binafsi, hivyo, tunapaswa kuwa makini na kupima matokeo ya athari zinazosababishwa na filamu zinazoweza kupatikana ama kwa mtu binafsi au watazamaji wote.

Mtazamo wa filamu za Magharibi, hasa Hollywood kuhusu nchi zinazoendelea ni wa kisiasa kabisa. Filamu hizo hutengenezwa kwa malengo maalumu na huweza kuacha athari miongoni mwa watazamaji.

Tafiti zilizofanywa zimeonyesha kuwapo ushawishi mkubwa wa filamu katika majukumu ya kijamii na mahusiano katika nchi zinazoendelea.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kwamba kama utamaduni wa asili utaridhia mahitaji ya watu, ni jamii ndogo tu ya watu itakayobaki imara kwenye maadili yanayotishiwa na vyombo vya habari vya kigeni.

Tafiti zingine kuhusu kubadilishana tamaduni zimegundua kwamba yatokanayo na vyombo vya habari vya Magharibi yanaongezeka katika kuleta athari kwa mtu mmoja mmoja, ingawa yana faida pia kama elimu na kuongezeka kwa uwezo wa uelewa.

Wakati vijiji na miji katika nchi zinazoendelea ikizidi kuwa na mtandao mpana wa upatikanaji wa filamu za Magharibi na video, nchi nyingi za Magharibi wana nafasi finyu sana ya kuona hali halisi ilivyo katika vijiji na miji ya nchi zinazoendelea ili kuwezesha kuwa na uelewa unaofanana.

Filamu za nje zinazopatikana Marekani nyingi hutengenezwa katika nchi za Ulaya, mara nyingi kwa ufadhili wa Marekani yenyewe.

Wachambuzi wengi wa nchi zinazoendelea wanahofu kwamba nchi zetu sasa zijiandae kupoteza kilicho chao na kupokea mambo na tamaduni za kigeni na kuwa katika hatari ya kuendeleza mazao ya Magharibi badala ya tamaduni zetu.

Utamaduni wa nchi ni “kidhibiti mwendo” kinachoongoza mwenendo na tabia za watu katika jamii, ni msingi wa maisha ya mtu binafsi kumwezesha kujitambua, kuwa na mwelekeo na kujichagulia falsafa sahihi ya maisha yake.

Nchi zinapaswa kuanzisha sera muhimu za kulinda haya ili kudhibiti umilikaji wa wageni wa kuagiza vitu toka nje, kupiga marufuku filamu zinazoingizwa kiholela, ukaguzi wa mara kwa mara, udhibiti wa maudhui ya filamu na tamthilia, na kutoa ruzuku kwa watengenezaji filamu wa ndani.

Kufuatia sera hizi umma uelimishwe kikamilifu juu ya sera hizi ili uweze kushiriki katika utekelezaji kwa upana wake. Pia ushirikishwaji wa vyombo vya habari katika kusaidia msukumo wa wananchi kuielewa sera ya utamaduni upewe nafasi ya kutosha.

Jambo muhimu na la msingi ni kuzingatia, kuzitambua na kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria.