Takwimu zilizotolewa zinaonyesha kuwa kutoka maambukizi 81,000 sasa yameshuka hadi 51,000 kwa mwaka.
Taarifa hizi ni njema kwa sababu wakati ugonjwa wa Corona ulipoingia nchini mwaka juzi watu wengi walisahau magonjwa mengine ya kuambukiza na nguvu kubwa ilienda katika kudhibiti virusi hivyo.
Nguvu iliyowekwa kudhibiti virusi vya Corona ilikuwa kubwa na kila mwananchi aliguswa kutokana na kasi ya maambukizi yake kusambaa kwa kiwango kikubwa na idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo kuwa mkubwa na kuitikisa dunia.
Tofauti ya maambukizi ya Corona na Virusi vya UKIMWI ni dalili za ugonjwa wa Corona kuonekana mara moja.
Wakati ugonjwa huo ukiingia nchini kuna waliosahau kama Virusi vya UKIMWI vinaendelea kushambulia watu kimya kimya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa TACAIDS, mwaka 2017, walipofanya utafiti waliona kiwango cha maambukizi kilifikia watu 81,000 kwa mwaka, lakini hadi kufikia mwaka 2021 wanakadiria kuwa watu 54,000 wanapata maambukizi mapya.
Kadhalika, katika utafiti unaofanyika kila baada ya miaka minne hadi mitano, pia imebainika hata vifo vimepungua kutoka watu 32,000 waliokuwa wanakufa kwa mwaka na kufikia watu 29,000.
Taarifa hiyo ya TACAIDS, inasema kiwango cha unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU kimepungua kutoka asilimia 28 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia tano.
Lengo la TACAIDS, ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kiwango cha maambukizi mapya ya VVU, vifo na unyanyapaa inakuwa ni asilimia sifuri kwa kuwa Tanzania bila UKIMWI inawezekana.
Takwimu hizi zilizotolewa na TACAIDS zinaonesha kuwa pamoja na nchi yetu kuwa katika janga la ugonjwa wa Corona, lakini watu wamekuwa na tahadhari ya kujilinda na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI ili kuliepusha taifa kuwa na watu wenye magonjwa hali inayoisababishia kutumia gharama kubwa ya kuagiza dawa.
Fedha hizo zinazotumika kuagiza dawa kutoka nje ya nchi zitumike kwa ajili ya mambo mengine ya maendeleo ambayo yatainua wananchi wa Tanzania kiuchumi na pia kulifanya taifa kuwa na rasilimali watu wenye nguvu ya kufanya kazi badala ya kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa.
Nguvu hiyo iliyotumika kupunguza idadi ya VVU, kupungua, iendelee kuhamasishwa maeneo mbalimbali nchini ili kila mmoja apate elimu ya kudhibiti ugonjwa huo.
UKIMWI unaua taratibu na mtu anapopata virusi hutumia gharama kubwa kuanzia kwenye dawa hadi lishe ili kuufanya mwili kuwa na nguvu. Dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI, zinahitaji mtu ale lishe bora itakayomwezesha kuhimili nguvu ya dawa hizo.
Kwa pamoja tukiendelea kutoa elimu ya kudhibiti ugonjwa huo tunaweza, na kama kaulimbiu ya TACAIDS inavyosema Tanzania bila UKIMWI inawezekana.









