TAKUKURU mulikeni ahadi za mil. 20/- ili Simba ifungwe

19Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
TAKUKURU mulikeni ahadi za mil. 20/- ili Simba ifungwe

LIGI Kuu Tanzania Bara imeanza kwa ushindani mkubwa msimu huu kila timu ikionyesha dhamira yake ya kuvuna pointi katika raundi hizi za mwanzo wakati huu ambao wiki hii inaingia raundi ya tano,...

... huku Yanga ikiwa kileleni kwa idadi tu ya mabao kutokana na kuwa na pointi 10 sawa na Simba na Namungo FC.

Tofauti na msimu uliopita, msimu huu klabu zimewekeza zaidi kwani hata zile ambazo zilizozoeleka kwa  kutokuwa na utamaduni wa kusajili wachezaji kutoka nje kama Klabu ya Tanzania Prisons na zingine, na zenyewe zimevuka mipaka ya nchi kufanya usajili.

Hii inaonyesha ni kwa namna gani kila timu ilivyodhamiria kufanya makubwa katika mbio hizo ubingwa wa ligi hiyo, ambayo msimu huu bonasi pamoja na zawadi zitaongezeka kutoka kwa wadhamini wa haki za matangazo, Kampuni ya Azam Media, lakini kuwania kukata tiketi ya michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu.

Hata hivyo, wakati mbio hizo zikiendelea kumezuka ahadi kwa timu mbalimbali kuahidiwa Sh. milioni 20 kama zitaifunga Simba na zikitoka sare Sh. milioni 10, zawadi ambazo tunazitilia mashaka na tunaona ipo haja ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuzimulika zisije kuwa chanzo cha upangaji matokeo.

Kinachotufanya kutilia hofu ahadi hizi ni kwanza, kwa nini zimekuwa zikitolewa kwa timu kutakiwa kuifunga Simba pekee na si zikicheza timu nyingine katika ligi hiyo?

Ikumbukwe ahadi hizi zilianza tangu msimu uliomalizika ambao Klabu ya Yanga ilitwaa ubingwa baada ya Simba kuubeba kwa misimu minne mfululizo, jambo ambalo limeanza tena kwa timu zinazocheza dhidi ya Simba.

Kwa kukumbusha tu katika mchezo wa kwanza wa Simba msimu wa 2021/22, wakati ikicheza ugenini dhidi ya Biashara United na mchezo kumalizika kwa sare tasa Septemba 28, 2021, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi, aliahidi kuipa timu hiyo Sh. milioni 20 endapo itaifunga Simba na Sh. milioni 10 ikipata sare.

Ahadi kama hiyo pia ilitolewa kwa Dodoma Jiji FC na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, kabla ya timu hiyo kuchezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri Oktoba Mosi, 2021.

Kama ilivyokuwa msimu uliomalizika kwa mechi hizo mbili za mwanzo, ambazo wadau na mashabiki walianza kupaza sauti na kuhoji kwa nini iwe dhidi ya Simba, na baadaye kimya cha ahadi za wazi kikatawala huku kukiwa na madai kwamba ziliendelea kutolewa kimya kimya, msimu huu tena zimeanza kusikika.

Katika mchezo wa kwanza msimu huu kwa Simba uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 17, mwaka huu kabla ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold FC, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Muhidin Michuzi, aliiahidi kuipa timu hiyo Sh. milioni 20 ikishinda na ikitoka sare Sh. milioni 10.

Kadhalika, siku moja tu baada ya kuingia mkataba wa kuidhamini Tanzania Prisons, Kampuni ya usafirishaji mizigo kwa njia ya bahari ya Silent Ocean, nayo ikatoa ahadi kama hiyo kwa klabu hiyo dhidi ya Simba ambayo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Septemba 14, mwaka huu.

Kwa ujumla Nipashe tunapenda kuona ahadi kama hizi zikizidi kutolewa kwa timu ama kwa wachezaji ili kuongeza ushindani na ligi yetu kuzidi kuwa bora zaidi, lakini hofu na mashaka yetu kwa nini zinatolewa dhidi ya timu inayocheza na Simba pekee na isiwe dhidi ya zinazocheza na Yanga, Azam, Namungo, Mtibwa na nyinginezo?

Hofu yetu kubwa kusije kukawa na viongozi wa timu kubwa ambazo zinaihofia Simba katika mbio za kutwaa ubingwa hivyo kuwatumia viongozi hao katika kuhakikisha wapinzani wao hawapati matokeo, na kwa njia hiyo inafahamika wazi huo ni upangaji wa matokeo jambo ambalo ni haramu na najisi kubwa katika soka duniani na ambalo litachafua ukuaji wa ligi yetu na soka la Tanzania kwa ujumla.

Hiivyo, tunaiomba TAKUKURU, kwa kutumia mkono wake mrefu, kumulika uhalali wa ahadi hizi ili kulinusuru soka letu lisitumbukie katika tuhumu za upangaji wa matokeo, lakini wawakilishi halali wanaoweza kuleta mafanikio chanya kwenye michuano ya kimataifa.