...inakamilika wikendi hii kwa timu sita za Tanzania kushuka dimbani, kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), kimeitwa kwa ajili ya kujiandaa na mechi mbili za kimataifa.
Mechi hizo za kirafiki za kimataifa zitachezwa katika kalenda rasmi inayotambulika na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), na Taifa Stars inatarajia kucheza dhidi ya majirani zao, Uganda (Cranes) na Waarabu wa Libya.
Ili kupata wachezaji kwa ajili ya kuitumikia Stars, ni lazima mchezaji uonyeshe kiwango kizuri katika mechi za mashindano yote ndani ya klabu yako, mchezaji unatakiwa utoe mchango kwa timu yao ili ifikie malengo iliyojiwekea katika msimu husika.
Kwa hapa nchini, wachezaji wa Tanzania watatakiwa kufanya vyema kupitia mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba na Yanga zote za jijini Dar es Salaam zinashiriki, sawa na wanaochezea KMKM ya Zanzibar.
Kwa upande wa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC ya jijini pia, Geita Gold FC kutoka mkoani Geita na Kipanga ya Zanzibar, wachezaji wake wanatakiwa kujituma ili kuwashawishi makocha wa Stars kuwaita kwenye kikosi chao.
Hakuna jambo lisilojificha kuwa mchezaji mwenye kiwango bora katika klabu yake ndio anayepata nafasi nzuri ya kuitwa kuvaa jezi ya taifa lake, hii haitaji kufanya mahesabu makali kama ya kuchanganya kemikali.
Katika kuhakikisha Stars inafikia malengo yake ya kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki na si kusindikiza mataifa mengine, ni lazima iite wachezaji wanaoonyesha viwango vya juu kwenye klabu zao.
Na hii si tu Stars inapokabiliwa na mechi za mashindano, hata pale inapokuwa na michezo ya kirafiki kwa sababu inapoibuka na ushindi, husaidia kuipa nchi pointi na hivyo kupanda kwenye orodha ya viwango vya ubora vinavyotolewa na FIFA kila baada ya miezi mitatu.
Hongera Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Honour Janza, kwa kuthubutu kuwaacha wachezaji waliokuwa wamezoeleka au wamejijengea himaya katika timu hiyo ili kuanzisha safari mpya ya matumaini ambayo imekuwa ni kiu cha muda mrefu cha Watanzania.
Mzambia huyo ameamua kuwaweka pembeni nyota kadhaa akiwamo nahodha wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Bakari Mwamnyeto, kiungo, Farid Mussa, Salum Aboubakari (Yanga), Jonas Mkude na Mohamed Hussein maarufu Zimbwe Jr na kuwaipa nyota wapya ili kuona timu hiyo inafika kule inapokuhitaji.
Inawezekana wachezaji hao wameachwa kwa sababu ya kushuka viwango vyao au hawajitumi kama ilivyotarajiwa na sasa nafasi wamepewa wachezaji wengine chipukizi au ambao wana uzoefu lakini walikosa namba kutokana na kushindwa kupambana na wakongwe hao.
Tunaamini wachezaji wapya walioitwa katika timu hiyo wanatakiwa kuonyesha bidii na juhudi kwa ajili ya taifa lao pia kutumia nafasi waliyoipata kujitangaza na hatimaye kujiongezea thamani.
Ni jambo lisilofichika mchezaji anapoonyesha kiwango bora ndani ya Stars anakuwa amejiweka katika daraja zuri atakaporejea kwenye klabu yake, lakini atazivutia timu nyingine mara dirisha la usajili litakapofunguliwa katika msimu unaofuata.
Lakini tunawakumbusha wale ambao wameachwa katika kikosi hicho kuendelea kupambana na hatimaye kurudi katika kikosi hicho kwa faida ya nchi na wao binafsi, wasikate tamaa kwamba wamekwisha, waamini timu ya taifa ni ya kila mtu na utaitwa pale tu kiwango chako kitakapokuwa kimelivutia benchi la ufundi na si vinginevyo.
Kufanya vizuri kwa Stars kutasaidia kuzivutia kampuni na taasisi nyingine mbalimbali kuwekeza katika mchezo huo pia kumpa heshima Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameongeza bajeti katika mchezo huo wa soka na mingine.
Kwa sasa wachezaji wa Stars wanapata huduma bora zinazostahili, nao imefika wakati wakarudisha furaha hiyo kwa Watanzania kwa kupambana kusaka matokeo bora, ingawa inafahamika katika soka kuna matokeo ya aina tatu.
Bila kusahau kuwatakia kila la heri wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo ya CAF ambao wanakamilisha mechi za hatua ya awali kwa kumaliza vyema na kusonga mbele.









