‘Panya road’ wanaweza kudhibitiwa

16Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
‘Panya road’ wanaweza kudhibitiwa

MAKUNDI ya panya road yanayoendelea kutishia maisha na usalama wa raia na mali zao yanaweza kudhibitiwa kama kutakuwa na nguvu ya pamoja.

Makundi hayo yanapoachiwa kuendelea kunyanyasa raia kwa kunyang’anya mali zao, kujeruhi na kufikia hatua mpaka ya kuua ni dalili mbaya na mnyororo wa matukio hayo utaendelea kukua.

Ni matukio mfululizo yametokea siku za hivi karibuni kwa makundi hayo kuvamia nyumba za watu, kufunga mitaa na kunyang’anya mali za watu.

Matukio hayo yanasababisha wananchi kuishi maisha ya hofu kwa sababu wakati mwingine yanatokea mchana kweupe.

Makundi ya panya road mengi yanaongozwa na vijana wadogo ambao hubeba silaha za jadi kama mapanga, visu na bisibisi na hufanya matukio ya uvamizi bila huruma.

Tumeona Bunge limeamua kulivalia njuga suala hilo kwa kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka na kwa uzito unaostahili, kuyakabili na kuyadhibiti makundi hayo ya kihalifu.

Hatua hiyo imetokana na baadhi ya wabunge, kuomba Bunge kuahirishwa na kujadili jambo la dharura, ambalo ni kukithiri kwa uhalifu unaofanywa na vikundi hivyo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mara na Singida.

Imeelezwa kuwa kuna wabunge tayari wamevamiwa na makundi hayo na kuathiriwa mali zao.

Jana, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliiagiza serikali kushughulikia jambo hilo kwa haraka, wakati alipokuwa akijibu mwongozo ulioombwa na wabunge wawili, Bahati Ndingo (Viti Maalum-CCM) na Mbunge wa Segerea (CCM), Bonna Kamoli.

Spika Dk. Tulia, alisema serikali ina uwezo wa kuchukua hatua kwa kuwa taifa lilishapata hizo changamoto na ilifanyia kazi na hayo mambo yakaisha kabisa. Hivyo, wanaamini hata hilo inao uwezo wa kulimaliza.

Hata hivyo, Spika Tulia amezungumzia hatua hiyo haitokani kwa sababu wabunge wameathirika, lakini kimsingi hata maisha yangeweza kuchukuliwa kutokana na kuwapo kwa walioumizwa na matukio hayo.

Spika alisema hata huko nje wananchi wanapata athari na kuitaka serikali ichukue hatua za haraka kushughulikia jambo hilo.

Wakati anasimama kuomba mwongozo huo, Mbunge wa Viti Maalum, Bahati Ndingo, alisema anaomba Bunge liahirishwe kwa muda ili kujadili jambo la dharura, kwa Kanuni ya 54, linalohusu suala zima la usalama wa raia.

Wabunge waliojenga hoja hiyo waliliambia Bunge kuwapo kwa taarifa mbalimbali katika Mkoa wa Dar es Salaam, kuhusiana na Panya road.

Panya road hao wamekuwa wakiendelea na uvamizi kwenye makazi ya watu na barabarani na juzi kusababisha mauti ya raia.

Hoja ya wabunge hao ni vikundi kama hivyo kuendelea nchini katika mikoa mingine kama Mara, wanajiita ‘Watu Kazi’ na wanaendelea na matukio hayo.

Wabunge hao waliomba kwa kuwa jambo hilo ni la dharura, unyeti wake, Bunge liahirishwe kwa muda waweze kulijadili na kuishauri serikali.

Juzi mwanafunzi mmoja anadaiwa kufariki dunia, baada ya watu zaidi ya 10 kuvamia nyumbani kwao, Kawe Mzimuni.

Mwanafunzi huyo alivamiwa na kusababishiwa kifo chake na wahalifu hao waliokuwa na silaha za jadi.

Kundi hilo la panya road lilivamia nyumba yenye vyumba 15 na kuvunja milango, kupora fedha, simu za mkononi, kujeruhi watu watatu na kumuua mtu mmoja.

Ni matumaini yetu kuwa suala hili kwa kuwa limefika bungeni, litapatiwa ufumbuzi ili liweze kukomeshwa na watu waishi kwa amani.