Mauaji yanayoendelea tatizo liko wapi

15Sep 2022
Mhariri
Nipashe
Mauaji yanayoendelea tatizo liko wapi

MATUKIO kadhaa ya mauaji yanayoendelea kutokea nchini ni dalili ya kuwapo kwa tatizo ambalo bado ufumbuzi wake haujapatikana.

Wingi wa taarifa za mauaji yanayotokea na kuripotiwa kila siku hazifurahishi na kuendelea kuleta masikitiko.

Watu wanaendelea kujitoa uhai na wengine kutoa uhai wa wenzao kwa jambo ambalo lingeweza kupatiwa ufumbuzi na kukomesha wimbi hilo kuendelea.

Jana wakati Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson akizungumzia suala hilo alilishauri Jeshi la Polisi kuangalia upya mfumo wao wa utoaji habari za mauaji, akionesha hofu pengine utaratibu unaotumika unachochea wengine kufanya vitendo hivyo.

Dk. Tulia alikuja na pendekezo hilo baada ya serikali kutaja vyanzo vya mauaji bungeni jana kipindi cha maswali na majibu kutokana na swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Cecilia Pareso aliyehoji kuhusu Tume iliyoundwa kuchunguza tatizo la mauaji ambayo ilitakiwa kutoa ripoti yake kwa umma na kuhoji pia lini serikali itakuja na mkakati wa kukabiliana na tatizo la watu kujichukulia sheria mkononi.

Wasiwasi wake ni kuwa pamoja na hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na tatizo hilo bado linaendelea kukua.

Hofu ya Spika ni utoaji wa taarifa unaweza kuwa kichocheo cha mwingine kuchukulia jambo hilo linawezekana na mwingine akafanya na kushauri kuangalia hatua zitakazosaidia kukomesha hali hiyo.

“Tukitumia hii sababu tu ya wivu wa mapenzi na nini, nadhani mtafute sababu za kawaida kabisa na mtuulize watu wa kawaida kabisa tunafikiri hilo jambo linaweza kumalizwa kwa namna gani.”

Spika alisisitiza polisi walitazame suala hilo kama wana haja ya kutangazia wananchi kila mauaji yanapotokea.

Ushauri wa Spika unaweza kuwa na mantiki, lakini Jeshi la Polisi pia lina wajibu wa kutoa taarifa kwa sababu wananchi wana haki ya kupata taarifa.

Inawezekana hapo nyuma taarifa hizo zilikuwa hazisikiki sana kutokana na wananchi kutokuwa na uelewa pale yanapotokea na kutotoa taarifa polisi. Lakini kadiri taarifa zinapotolewa ndivyo wananchi wanavyokuwa na uelewa wa kuripoti matukio hayo na kufahamika kwenye jamii.

Kuyakalia kimya maana yake ni kuficha ukweli wa tatizo ni bora yatangazwe ili iweze kupatikana dawa ya kuyadhibiti.

Kuna matukio ya ubakaji hapo nyuma yalikuwa hayaripotiwi kama yanavyoripotiwa sasa kwasababu ya watu kuwa na uelewa.

Taarifa hizo ziliibuka kwa wingi na baadhi ya wadau wakaanza kuhoji pengine yanavyoripotiwa ndiyo yanashawishi watu wengine kuyafanya.

Lakini, ukitafakari ni kuwa mwanzo yalikuwa hayaripotiwi kwa wingi kutokana na kufumbiwa macho na baadhi ya familia kuyamaliza kimyakimya kwa kulipana fidia.

Baadhi ya watu wanakosa uelewa wa kutambua jambo lipi baya na lipi zuri mpaka atakapopata elimu ya kutambua hilo.

Vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa wa kutoa elimu na watu kufunguka kwa kutambua umuhimu wa kutoa taarifa yanapotokea matukio ambayo hayapendezi katika jamii.

Ni jambo la muhimu kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ili watu wasiendelee kuangamia kwa kukosa msaada wa kulitatua tatizo.