Kupitia uteuzi huo, imeshuhudiwa wanawake waking’ara katika kila uteuzi unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwamo mawaziri na manaibu wao, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri.
Licha ya nafasi hizo, hivi karibuni ilishuhudiwa Rais Samia akiwateua majaji wengi wanawake katika Mahakama Kuu ya Tanzania jambo ambalo lilipongezwa na wadau mbalimbali wakiwamo wanaharakati wa haki za binadamu. Hatua hiyo ya uteuzi wa wanawake katika nafasi mbalimbali inalenga kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 katika ngazi za uamuzi.
Aidha, juzi wakati akifungua mkutano wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kuhusu Wanawake na Vijana katika Biashara jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema Sheria ya Ununuzi wa Umma imetoa nafasi kwa wanawake kupewa kipaumbele katika miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali.
Kupitia miradi hiyo, Rais alisema asilimia 30 ya miradi hiyo itatolewa kwa kampuni zinazomilikiwa na wanawake, lengo kubwa likiwa kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kuwa na uwezo katika umiliki wa uchumi.
Sambamba na hilo, pia serikali imeanza kubadilisha baadhi ya sheria kandamizi zikiwamo zile zinazowanyima fursa wanawake kufanya shughuli kwa amani pamoja na kuondoa vikwazo vinavyowakabili, vikiwamo unyanyasaji wa kijinsia katika biashara.
Pia serikali, katika kuhakikisha azma hiyo inatimia, imezitaka taasisi za kifedha zikiwamo benki kuanzisha madirisha maalum kwa ajili ya mikopo kwa wanawake itakayotolewa kwa riba na masharti nafuu ili kuwaongezea ukwasi na kutimiza ndoto zao za kimaendeleo hasa katika utekelezaji wa miradi ambayo wanapata kazi.
Kwa ujumla, hatua hiyo ya kuwawezesha wanawake ni nzuri na inastahili kuungwa mkono kwa kuwa wanawake ni moja ya makundi ambayo yamekuwa nyuma kimaendeleo kwa muda mrefu kutokana na mfumo dume uliokuwa umeshamiri kwa miaka mingi. Ni imani kwamba wanawake wanapowezeshwa kiuchumi, watatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa.
Kutokana na mipango hiyo, ni wakati sasa kwa wanawake kuamka na kuchangamkia fursa hizo za kimaendeleo ikiwamo kuungana na kuanzisha shughuli za kibiashara kwa wale ambao hawajaanza. Kwa wale ambao wameshaanza kupitia vyama na mashirikisho yao, wanapaswa nao kuhakikisha fursa hizo haziwapiti.
Kama alivyosema Rais Samia, kuna miradi mingi kama vile ujenzi wa barabara vijijini na usambazaji wa maji ambapo kampuni za ujenzi na uhandisi zinazomolikiwa na wanawake zinaweza kutekeleza. Wakati ni sasa kwa wanawake kuchangamkia fursa hizo.
Pamoja na hayo, wanawake waonyeshe kuwa wanaweza wanapopewa nafasi hizo kwa kufanya kazi zenye viwango vya kuridhisha na hatimaye kuifanya serikali kuwaongezea zaidi kazi na hatimaye kunufaika kiuchumi na kijamii.