Maelekezo hayo ni kushughulikia malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza kuhusu gharama za tozo za miamala ya kielektroniki ili kuleta unafuu.
Kilio cha tozo kimewaibua wadau kutoka nyanja mbalimbali kuhusu mzigo wa tozo wanazotozwa wananchi na wengine hata kudiriki kutoa kauli za kukata tamaa ya kuhifadhi fedha katika benki kwa hofu ya tozo hizo.
Wengi wamekuwa wakihoji iweje mtu anapokwenda kuhifadhi fedha zake mahala salama, akatwe kodi na anapokwenda kuzitoa pia akatwe.
Wengine walikuwa wakilalamika wanapokwenda kulipa ushuru Mamlaka ya Mapato (TRA), pia anatakiwa aulipie tozo.
Hakika kilio kilikuwa kikubwa kuanzia kwa wananchi mmoja mmoja, mitandao ya kijamii na hata kwenye mikusanyiko ya watu.
Waziri wa Fedha Dk. Nchemba akiwa wilayani Tarime mkoani Mara katika ziara ya kikazi alitoa kauli hiyo ya kushughulikia kilio cha tozo wakati akizungumza na wananchi, wafanyabiashara na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA.
Aliahidi kuwa wataalamu wa wizara yake wanayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Rais, Chama Tawala (CCM) pamoja na maoni ya wananchi na kwamba muda si mrefu serikali itakuja na majawabu baada ya kufanya marekebisho ili kuleta unafuu.
Kwa wananchi tunasema hatua hii ni nzuri na inatia faraja kuona Rais wetu ni msikivu kwa kusikia kilio cha wananchi wake.
Watanzania wamejenga imani kwa Rais wao kwa kuwa wanajua ni msikivu ndiyo maana kilio cha tozo kilikuwa hakiishi midomoni mwao wakijua atasikiliza na amedhihirisha hilo kwa kuagiza lifanyiwe kazi.
Tozo huleta maendeleo katika nchi yoyote duniani, lakini ziangaliwe ili zisimuumize mwananchi ili naye aweze kufurahia anapoitoa akijua italeta faida.
Akifafanua kuhusu ukusanyaji wa mapato kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Waziri wa Fedha anasema unaenda sambamba na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuweka miundombinu wezeshi inayolenga kuibua wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa na hatimaye kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Pamoja na serikali kuhitaji fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali, lakini hata matumizi ya fedha hizo pia yaangaliwe kwa kuwa kilio kikubwa cha wananchi ni utumiaji unaozidi kiwango.
Wengi wanaolalamika wanadai matumizi makubwa serikalini kuanzia magari ya gharama ya viongozi na mambo mengine yanachangia kuleta malalamiko.
Hata baadhi ya miradi inayotekelezwa kuonesha kutumia fedha nyingi kuliko uhalisia wa mradi wenyewe.
Juzi tu Waziri Mkuu alipokuwa katika ziara, aligundua kibanda cha mlinzi na nyumba za watumishi wa umma kugharimu fedha nyingi katika ujenzi na kuamuru ufuatiliaji.
Mambo kama hayo huibua malalamiko na maswali kutoka kwa wananchi ambao hubeba mzigo wa kulipa tozo.









