Simba, Yanga jipangeni CAF kwa 90 zingine, kazi haijaisha

12Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga jipangeni CAF kwa 90 zingine, kazi haijaisha

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga kwa upande wa Tanzania Bara, wameanza vizuri mechi zao za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini huzuni kubwa ni kwa Tanzania Visiwani kutokana na KMKM kuanza kwa kuangukia pua nyumbani.

Simba ikiwa ugenini nchini Malawi juzi, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao, Nyasa Big Bullets, wakati Yanga ambayo kikanuni nayo ilikuwa ugenini licha ya mchezo wao dhidi ya Zalan FC kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ilitoka na ushindi mnono wa mabao 4-0.

Zalan FC ya Sudan Kusini, iliutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kama wao wa nyumbani kutokana na hali ya usalama nchini kwao kutokuwa shwari, hivyo mechi ya marudiano Jumamosi wiki hii, itapigwa tena uwanjani hapo Yanga sasa ikiwa mwenyeji.

Balaa kubwa siku hiyo kwa wawakilishi wengine wa nchi kwa upande wa Tanzania Visiwani, timu ya KMKM, ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Al Ahli Tripoli ya Libya, hivyo mchezo wa marudiano itakuwa na mlima mrefu wa kubadili matokeo hayo ili kusonga mbele.

Hata hivyo, bado tunaamini hakuna kinachoshindikana ndani ya dakika 90, kwani kama Al Ahli Tripoli iliweza kuibuka na ushindi huo ugenini, pia KMKM inaweza 'kupindua meza' nchini Libya kama ikijipanga vizuri na kurekebisha ilipokosea, kwa kuwa tayari inamjua vema mpinzani wake.

Lakini pia katika hilo, kwa Simba na Yanga, hazipaswi kubweteka kwa matokeo mazuri ziliyopata kwani tulishawahi kushuhudia wapinzani wao wakija hapa nchini na kupindua meza kutokana na wenyeji kuamini tayari wameshamaliza mchezo.

Hilo linatufanya kuwaonya wawakilishi wetu hasa tukikumbuka Agosti 10, 2019, wakati Simba ilipotoka sare tasa ugenini dhidi ya UD Songo ya Msumbiji na katika mechi ya marudiano Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati huo Luis Miquissone akiichezea UD Songo, akaipatia bao la kuongoza dakika 12, lililodumu hadi dakika ya 87 Erasto Nyoni aliposawazisha kwa mkuju wa penalti, hivyo kuwafanya wageni hao kusonga mbele kutokana na faida ya bao la ugenini, safari ya Simba ikiishia hapo.

Kadhalika, Oktoba 17, mwaka jana katika michuano hiyo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na kurejea nchini kifua mbele ikiamini imemaliza mchezo na wanachokisubiri ni kukamilisha ratiba tu kabla ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Kilichowakuta katika mchezo wa marudiano Oktoba 24, 2021, hakuna aliyeamini baada ya mashabiki, wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa vichwa chini kutokana na kukubali kichapo cha mabao 3-1, hivyo kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Mifano hiyo hai ya hivi karibuni, ndiyo inayotufanya kuzionya Simba na Yanga, tukizitaka kuchukua tahadhari mapema kwa kuingia uwanjani katika mechi za marudiano zikiamini bado mchezo haujaisha hadi dakika 90 za pili zitakapomalizika wakiongoza kwa jumla ya mabao ya nyumbani na ugenini.

Pamoja na mtaji mkubwa kwa Yanga ilionao wa mabao 4-0, na ule wa Simba wa magoli 2-0, bado haitoshi kuwa sababu ya kubweteka katika mechi za marudiano, kwani katika mchezo wa soka ukifanya makosa tu unaadhibiwa jambo ambalo linaweza kutokea wakati wawote kama wachezaji hawatajengwa kisaikolojia kwa kujazwa ari ya kupambana mwanzo mwisho.

Sisi tunatamani kuona Tanzania kwa mara ya kwanza inaweka rekodi ya kuingiza timu zote tatu; Simba, Yanga na KMKM katika hatua ya makundi na hilo linawezekana tu kama kila mmoja kuanzia mashabiki, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi watatimiza wajibu wao nje na ndani ya uwanja.

Tunaamini mabenchi ya ufundi ya wawakilishi wetu hao kimataifa, wameona ulipo ubora na udhaifu wa wapinzani wetu kama ambavyo nao tayari wamewaona, hivyo kinachotakiwa ni kufanya kazi ya ziada kwa siku hizi sita zilizobaki kabla ya mechi za marudiano.

Na katika hilo, mashabiki na Watanzania kwa ujumla hatuna budi kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi kuipa sapoti Yanga dhidi ya Zalan FC na Jumapili wakati Simba itakapoikaribisha Nyasa Big Bullets ya Malawi.

Tunatambua shabiki siku zote ni mchezaji wa 12 uwanjani, hivyo Watanzania 60,000 tu wanahitajika kujitokeza kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi na Jumapili ili kuwapa sapoti wawakilishi wetu hao waweze kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo inayoongoza kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.