Simba, Yanga, Azam kila la kheri mashindano CAF

10Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga, Azam kila la kheri mashindano CAF

MSIMU mpya wa mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho katika hatua ya awali yanatarajiwa kufanyika kuanzia leo katika viwanja mbalimbali hapa barani Afrika.

Tanzania katika mashindano hayo yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), inawakilishwa na jumla ya timu sita, nne kutoka Bara na klabu nyingine mbili kutoka Zanzibar.

Kwa upande wa Tanzania Bara, Simba na Yanga zote za Dar es Salaam zinatarajiwa kuanza kupeperusha bendera zake leo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam FC ya jijini pia na Geita Gold FC ya mkoani Geita zenyewe zitachuana kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 Zanzibar katika michuano hiyo ya kimataifa itawakilishwa na KMKM inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kipanga FC wao watapambana kuwania ubingwa wa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika kuhakikisha zinakwenda kushindana na si kusindikiza wengine, timu zote hizo zimefanya usajili mzuri kwa kuzingatia mapungufu waliyoyaona katika msimu uliopita, maana yake wameimarisha vikosi vyao kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Wawakilishi hawa wamefanya pia maandalizi yanayostahili katika kipindi cha Pre Season, lakini pia walicheza michezo mbalimbali ya kirafiki dhidi ya timu za ndani na nje ya nchi ili kujiweka imara na tayari kwa mapambano hayo.

Mbali na mechi hizo za kirafiki, kwa upande wa Simba, Yanga, Azam na Geita Gold zimepata nafasi ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo zitakuwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea michuano hiyo ya CAF, ambapo makocha wanaweza kutumia michezo hiyo kuimarisha wachezaji pale walipobaini kuna matatizo.

Timu zote nne zimepata mechi ngumu kwa sababu kila timu walizokutana nazo zilikuwa zinahitaji kuvuna pointi, hivyo kwa maana nyingine zimewapa maandalizi mazuri wawakilishi hao wa nchi katika mashindano ya kimataifa.

Pia kwa upande wa Zanzibar, KMKM na Kipanga zimepata nafasi ya kushiriki michuano maalumu ya Pre Season na vile vile zimecheza mechi moja za ligi, na kwa umuhimu wake, ilitumia nyota wake wote muhimu kuwaweka tayari kwa sababu zilifahamu majukumu ya kimataifa yaliyokuwa mbele yao.

Tunawakumbusha wachezaji wa timu zote sita kucheza kwa bidii, kujituma wakati wote na kufahamu wanatakiwa kutumia michuano hiyo kutimiza ndoto zao za kupata klabu za nje na hatimaye kuongeza idadi ya nyota wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa.

Wachezaji wafahamu wanatakiwa kupambana kusaka matokeo chanya katika mechi hizi za kwanza na kujiweka kwenye nafasi nzuri kuelekea michezo ya marudiano, haijalishi timu inaanzia nyumbani au ugenini.

Lakini kama ambavyo tumeshuhudia klabu za Tanzania zikisajili wachezaji waliofanya vizuri na wapinzani waliocheza nao, huu ni wakati mwingine sahihi wa nyota wa Kitanzania kujiweka sokoni na hatimaye kuwavutia makocha wa timu za nje. Tunaamini kama Simba, Yanga na Azam zinasajili kutoka kutoka Uganda, Rwanda, Kenya, Zambia, Malawi au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tunataka kuona timu za nje nazo kupitia michuano ya msimu huu zinavutiwa na wachezaji Watanzania kama vile walivyosajiliwa kina Mbwana Samatta, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Kelvin John, Abdi Banda na wengineo.

Timu inapopata ushindi katika mechi yake ya kwanza hupunguza presha kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wake kuelekea mchezo wa marudiano ambao tayari kila mmoja anakuwa ameshamfahamu vyema mpinzani wake.

Tunafahamu kila hatua huwa na dakika 180, lakini ni vyema kila klabu ikajidhatiti kuhakikisha inamaliza kazi ndani ya dakika 90 za kwanza na kuacha muda uliobakia kuwa mwepesi na si wenye mawazo.

Tunawakumbusha hivi kwa sababu tunahitaji kuona timu za hapa nchini zinafika mbali katika mashindano hayo na kufuta usemi uliozoeleka wa 'Kichwa cha Mwendawazimu' na kuonekana klabu za Tanzania ni tishio.

Tunapenda kuzitakia kila la kheri timu zote za Tanzania katika mashindano hayo ya CAF ambayo ni makubwa Afrika kwenye ngazi ya klabu.