Agizo la Waziri Ummy matibabu bure litekelezwe

08Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Agizo la Waziri Ummy matibabu bure litekelezwe

JANA Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alikuwa mjini Kibaha, mkoani Pwani na kuagiza vituo vya afya vya serikali kutoa huduma bure kwa watu wanaokwenda kutibiwa ugonjwa wa malaria.

Pia aliagiza wanaokwenda kufanya vipimo vya ugonjwa huo na kifua kikuu wasitozwe fedha.

Hatua hiyo ya Waziri Ummy imetokana na ziara yake ya siku moja aliyoambatana na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa (Global Fund) wa kusaidia mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (HIV), kifua kikuu (TB) na Malaria, Peter Sand, aliyefika kujionea huduma zinazotolewa na vituo hivyo.

Mfuko huo unasaidia Tanzania kutokomeza magonjwa ya malaria, kifua kikuu na Ukimwi.

Ugonjwa wa malaria ni miongoni mwa magonjwa matano nchini unaoongoza kwa kusababisha vifo.

Hivyo, hatua ya Waziri Ummy kuagiza vituo vya afya vya serikali kutoa huduma bure kwa wagonjwa wa malaria, itasaidia kupunguza vifo.

Ni kweli baadhi ya watu wanashindwa kwenda vituo vya afya kwa kutokuwa na fedha za matibabu na vipimo na kuishia kununua dawa za kutuliza maumivu au kwenda kwa waganga wa jadi.

Magonjwa yaliyotajwa na Waziri Ummy ambayo yanapaswa kutolewa huduma bure, ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo nchini.

Kwa mfano, ugonjwa wa malaria humaliza damu kwa muda mfupi na mtu asipopata matibabu kwa wakati, hupoteza maisha.

Magonjwa kama kifua kikuu na Ukimwi, dawa zake ni kali hivyo mtu anahitaji kula chakula cha kutosha ili asiweze kupata madhara.

Ukiangalia baadhi ya watu wanaougua maradhi hayo, wanakosa uwezo wa matibabu na lishe nzuri. Hivyo hatua hiyo ya kutoa huduma hiyo bure itawasaidia wananchi wengi ili pesa ambayo alikuwa aitumie kwenye matibabu imsaidie kununua lishe bora.

Kwa wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa wa Ukimwi (ARV), wanahitajika kula vizuri ili miili yao iweze kujijenga na kuwa na afya njema.

Ummy, katika ziara hiyo alitahadharisha wanaosuasua kutumia dawa za ARV kwa wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kuwa ni hatari kwao kwa sababu maambukizi yanasambaa kwa kasi.

Anasema katika watu 100 nchini wanaoishi na virusi vya Ukimwi, 95 wanaotumia dawa wanasuasua kwa kujiona wapo vizuri na hivyo kuacha kutumia.

Aliwakumbusha kuwa hata kama wanaona hawaumwi, wasiache kutumia dawa.

Ni matumaini yetu kuwa agizo hili la Waziri Ummy litatekelezwa ili wagonjwa wanapokwenda kupata huduma wasipate usumbufu.

Uzoefu unaonesha kuwa maagizo mengi yanapotolewa utekelezaji wake huchukua muda na wale wanaohitaji huduma kuona kama wananyanyasika na kudharauliwa.

Utaratibu wa kuviongoza vituo hivyo ufanyike kwa wakati ili vifo vitokanavyo na magonjwa hayo vizuilike.

Mkurugenzi wa Global Fund Peter Sand, akizungumzia mfuko huo alisema ameridhishwa na huduma zinazotolewa hususani kukabiliana na magonjwa ya Ukimwi, malaria, kifua kikuu na huduma za mama na mtoto.

 

Alihikikisha kuwa mfuko huo utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza mapambano dhidi ya kifua kikuu, HIV, maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na malaria.