Si hivyo tu, wapo wanaoingiwa na hofu zaidi kwa kuwa hata sasa wanakabiliwa na njaa kwa vile wanakula mlo mmoja tena unaopatikana kwa taabu.
Ni kweli kuwa kuna ugumu wa maisha unaotokana na sababu nyingi zikiwamo kupanda kila wakati kwa bei ya mafuta, kunakopandisha bei za kila kitu kuanzia bidhaa za viwandani, chakula hadi nauli ni mambo ambayo yanawafanya wengi kukosa utulivu, amani moyoni pamoja na matumaini.
Hivi karibuni uhaba wa mvua hasa za masika umewafanya wakulima wengi kuvuna haba lakini walaji nao kukosa chakula kwa bei nafuu sokoni na kukabiliwa na njaa .
Ni kutokana na ukame kwani mikoa mingi haikuvuna nafaka za kutosha hasa mahindi, mpunga, lakini pia maharage, kunde na mengine yanayofanana na hayo hayakupatikana kama ilivyotegemewa.
Kitisho kipya cha ongezeko la bei ya vyakula masokoni kinachoshuhudiwa sasa ni matokeo ya mambo mengi kuanzia ughali wa mafuta, ukame ulioharibu mazao, kufa mifugo lakini pia mafuriko yaliyoharibu mazao na kusababisha njaa, hivyo hakuna wa kulaumiwa moja kwa moja.
Kupanda kwa bei ya chakula na watu wengi kukosa akiba ya chakula nyumbani pia wakishindwa kukinunua sokoni inamaanisha kuwa kuna dalili za njaa ambayo ni shida kubwa ya chakula kwa jamii kubwa.
Uhaba wa chakula na kuongezeka kwa bei za vyakula unamaanisha kuwa familia nyingi zitakuwa kwenye hali ngumu hasa zile ambazo zina kipato kidogo ambao ndiyo Watanzania wengi waishia mijini na vijijini.
Njaa haina macho lakini inapotokea wanaoathirika zaidi ni watoto, wahitaji, wasiojiweza hasa kaya maskini, watoto wachanga na watoto ambao wengi ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ni mbaya zaidi.
Tunakumbusha kuwa kupanda kwa bei ya chakula kunamaanisha njaa kwenye kaya kwa vile nyingi zitakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Aidha, pia watu hasa watoto watapata utapiamlo na hali inapokuwa mbaya wanazidi kuwa na udhaifu. Hilo linatokana na lishe duni na magonjwa nyemelezi ni rahisi kuleta vifo.
Yote hayo ni kutokana na uhaba wa chakula na ughali masokoni.
Tunaamini kuwa serikali imesikia na inaona pia, tukiamini haitachelewa kulitupia macho suala la ughali wa vyakula kwa kuwa ni tatizo kwa watu wote.
Ikumbukwe kuwa watoto kukosa chakula kutasababisha hata wengine kupata utapiamlo unaosababisha kudumaa akili kuchelewa kukua, kuwa mbumbumbu na kuongeza tena gharama za kuihudumia jamii inayoathirika.
Kukiwa na watu waliokosa vyakula au wenye njaa kunamaanisha kuwa taifa litapata tena gharama za kulisha watoto waathirika hasa wa unyafuzi, udumavu watakaolazwa mahospitalini. Kadhalika kwenye elimu litakabiliwa na kazi ya kuhudumia wenye mahitaji maalumu madarasani.
Tunaishauri serikali kuliangalia suala la ongezeko la bei ya nafaka na kuchukua hatua kwa kuwa tatizo hilo lina athari kubwa kwa Watanzania zaidi ya asilimia 90, ikimaanisha kuwa walio wengi wataumia kwa njaa iwapo hali haitadhibitiwa.
Ni ushauri wetu kwa mamlaka za chakula,wabunge na wadau wengine wa kilimo na usalama wa chakula wachukue hatua wasikae kimya, waeleze ni nini cha kufanya na hata ikibidi kuangalia uwezekano wa kutumia utaratibu wa bei elekezi.
Tunakumbusha kuwa kama ambavyo serikali ilifanya kwenye mafuta iangalie uwezekano wa kutoa ruzuku kwa wafanyabiashara wa nafaka wakiwamo wasindikaji wa mahindi na ngano lakini pia wauzaji wakuu wa mpunga ili kupunguza ukali wa tatizo.
Yapo madai ya kufunguliwa mipaka na vyakula kuuzwa nje kwa kiasi kikubwa hilo nalo, tunaiomba serikali ilitupie macho na kutoa maelekezo ambayo hayatawaumiza aidha wakulima au kuleta shida ya vyakula kwa wananchi.









