Takwimu zinaweza zisipatikane zote kutokana na matukio mengine kutoripotiwa kwa sababu mengine sio rahisi kuripotiwa kwa kuwa yanatokea bila watu wengine kujua.
Matukio mengi ya mauaji yanayoripotiwa sababu zinazotolewa ni kutokana na wivu wa mapenzi, mali, ushirikina na mambo mengine ya kifamilia.
Watu wanaofanya mauaji hayo wanatoka kwenye familia hizohizo, jambo ambalo linazua maswali mengi.
Jamii imekuwa ikijiuliza watu wamekuwa wanyama kiasi hicho na kwanini sasa matukio haya yanaendelea kushamiri kila siku pamoja na dola kutoa adhabu kali kwa wanaokutwa na makosa ya vitendo hivyo?
Wanasaikolojia mara nyingi wamekuwa wakitoa elimu ya dalili za watu ambao wanaonekana kuwa na utofauti wa maisha na wengine kufikia hatua ya kuchukua uamuzi huo wa mauaji.
Baadhi ya matukio ukiyafikiria unaweza ukashangaa kama aliyefanya alikuwa na akili timamu au kuna tatizo la afya ya akili.
Wengine huchukua uamuzi wa kujiua wenyewe kwa sababu zinazotolewa za ugumu wa maisha, msongo wa mawazo au kuchoshwa na magonjwa yanayomkabili.
Ndiyo maana wanasaikolojia wanatahadharisha jamii kuwa makini na watu wanaowaona kuwa na mabadiliko katika mienendo yao kama vile kujitenga na watu, kuwa mlevi wa kupindukia, mtu mwenye mawazo na wakati mwingine kutoa matamshi ya kutaka kujiua.
Katika baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni yanayohusu mauaji, ni tukio la binti aliyekutwa ameuawa na mwili wake kutupwa barabarani na watu wasiojulikana. Mwili wake pia ulikutwa pembeni ukiwa na chupa ya kilevi. Kwa nini ameuawa ni maswali ambayo wengi wanajiuliza.
Lakini, matukio yanayosikitisha zaidi ni ya ndugu wa karibu wakiwamo watoto kuua wazazi kwasababu ya kuwahisi ni wachawi au kutaka kurithishwa mali.
Tukio ambalo limeshangaza ndugu wa familia moja huko wilayani Masasi, mkoani Mtwara ni la mtoto kutuhumiwa kumuua baba yake mzazi kisa kikidaiwa kuwa aliwataka wamtafutie mchumba na alipoona ombi lake halijafanyiwa kazi akaamua kuchukua uamuzi huo wa kuondoa maisha ya mzazi wake mmoja huku akimwachia majeraha mama yake.
Ukijaribu kufikiria utaona kabisa hapa kuna tatizo la afya ya akili ambalo linatakiwa lifanyiwe kazi kuanzia kwenye ngazi zetu za kifamilia.
Katika kipindi fulani kulikuwa na matukio ya kushamiri kwa ajali za bodaboda, lakini uchunguzi ulipofanyika ikabainika kuwa baadhi ya madereva wa vyombo hivyo hutembea na vilezi na kuvitumia wawapo kwenye shughuli zao.
Vivyo hivyo, kunahitajika ushirikiano wa hali ya juu wa kujichunguza katika familia zetu kuona umuhimu wa kuangalia afya zetu za akili ili matukio haya ya mauaji yaweze kudhibitiwa.
Jamii ndiyo yenye jicho la kwanza kumbaini mwenzake kutokana na mabadiliko atakayoyaona toka kwa mwanajamii mwenzake.
Kama taarifa itatolewa mapema na mtu huyo akachunguzwa na hata kumzungumza naye inaweza kusaidia kumwepusha na dhamira anayotaka kuichukua.
Wanajamii ni watu muhimu sana katika kutoa msaada kwa wenzao ili kunusuru janga kubwa lisiweze kutokea. Kwa pamoja tunaweza kudhibiti hali na pia maofisa Ustawi wa Jamii mnajukumu kubwa ni elimu ili kudhibiti vitendo hivi kuendelea kutokea.









