Wawakilishi wetu CAF malizeni kazi mapema

05Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wawakilishi wetu CAF malizeni kazi mapema

AWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa kwa upande wa klabu, Simba, Yanga na Geita Gold Jumamosi na Jumapili wiki hii, watashuka katika viwanja tofauti ndani na nje ya nchi kuanza kuwania kupeperusha vema bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba na Yanga zinaiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa wakati Geita Gold na Azam FC ambayo yenyewe itaanzia raundi ya kwanza, zikiwa na jukumu la kuipeperusha vema bendera ya taifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wa Simba, itaanzia ugenini Jumamosi wiki hii dhidi ya Nyasa Bigi Bullets ya Malawi, wakati Yanga yenyewe ikiangukia bahati ya mtende baada ya Zalan FC ya Sudan Kusini, kuomba mechi zake zote mbili kuchezwa hapa nchini katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Zalan FC ambayo mchezo wa Jumamosi itakuwa mwenyeji, imeomba kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kutoka na hali ya usalama nchini kwao kutokuwa shwari.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Geita Gold itaanzia ugenini nchini Sudan dhidi ya wenyeji wao, Hilal Alsahil, katika mchezo utakaopigwa Jumapili wiki hii kabla ya timu hizo kurudiana nchini Jumamosi ya juma lijalo.

Kwa ujumla michuano hii inahitaji mahesabu makali kwa kila timu kuchanga karata zake vizuri ili kuweza kuvuka hatua hii ya awali kwenda raundi ya kwanza ambayo kwa timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa zitakuwa na faida kubwa ya kuweza kuendelea kuchuana kimataifa hata zikipoteza.

Hii ni kutokana na kanuni ya mashindano hayo, kutoa faida kwa timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa ambazo zitatolewa katika raundi ya kwanza (baada ya hii ya awali), huangukia kwenye mechi za mchujo za Kombe la Shirikisho na zikishinda hutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa utajiri kwa ngazi za klabu barani Afrika.

Hivyo, kinachotakiwa kwanza ni Simba na Yanga kuelekeza malengo yao kwenye kuendelea kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa kuhakikisha zinafanya vizuri kwenye mechi zao za awali ugenini kwa kupata ushindi mnono ili kurahisisha kazi katika michezo yao ya marudiano mwishoni mwa wiki ijayo.

Tunatambua si kazi rahisi kwa kuwa timu zote zilizotinga hatua hiyo ni zile zilizofanya vizuri kwenye ligi zao za ndani, lakini kutokana na usajili wa maana wa klabu zetu hadi maandalizi zilizofanya, tunaamini hakuna kinachoshindikana kama kila mmoja kwa nafasi yake atajitoa kikamilifu kutekeleza majukumu yake kuanzia viongozi wa timu hizo, mabenchi ya ufundi, wachezaji hadi mashabiki.

Wakati huu ambao barani Afrika bado kanuni ya timu kufaidika kwa bao la ugenini ikitumika, ni wakati muafaka kwa wawakilishi wetu hao wa nchi kuitumia vema katika mechi zao hususan ni raundi hii ya awali ambayo zote zinaanzia ugenini.

Kinachotakiwa ni kuhakikisha yanapatikana mabao mengi na kutokubali kuruhusu nyavu zao kutingishwa ili michezo ya marudiano hata kama zikiambulia sare ya aina yoyote ile, ziwe na uhakika wa kutinga raundi ya kwanza.

Lakini katika kufanikisha hilo, ni wakati wa mashabiki kujitoa bega kwa bega kuongozana na timu zao ugenini kwenda kuzipa sapoti kwani tunaamini siku zote shabiki wa soka ni sawa na mchezaji wa 12 uwanjani, pale anapojitokeza kuishangilia mwanzo mwisho.

Kwa hatua hii ya awali ambayo Simba na Geita Gold FC zitakuwa ugenini, tunaamini kwa mashabiki kujipanga kwenda Malawi ama Sudan, wanaweza kabisa kumudu gharama hizo, jambo ambalo litaonyesha mapenzi makubwa na nia ya dhati ya kuziunga mkono klabu zetu.

Lakini kwa mashabiki wa Yanga na Watanzania kwa ujumla, huu ni wakati wa kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuipa sapoti klabu hiyo katika michezo miwili itakayocheza nchini dhidi ya Zalan FC.

Tunatambua wapo ambao wanaweza kuibeza Zalan FC kwa kuiona ni timu ya kawaida kutokana na nchi inayotoka kuwa chini kisoka ukilinganisha na Tanzania, jambo ambalo hatuna budi kuwaonya wachezaji wa Yanga na benchi la ufundi kwa kutoichukulia 'poa' timu hiyo kwa kuwa siku zote mchezo wa soka huwa na matokeo ya kushangaza.

Hivyo, kwa muda huu wa siku takriban nne zilizobaki kabla ya mitanange hiyo kupigwa, tunawatakia maandalizi mema wawakilishi wetu, lakini tukiamini makocha watatumia muda mfupi kuziba panapovuja na kuwajenga zaidi wachezaji wao kisaikolojia.