Katika marekebisho hayo, serikali imepunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi 50, kulingana na kundi la miamala.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alitangaza hatua hiyo ya serikali baada ya kusema imefanya mapitio na kupunguza mzigo wa tozo kwa jamii ili kuchochea matumizi ya miamala kwa njia ya fedha tasilimu, kurahisisha utozaji na kuzuia utozaji wa tozo husika mara mbili.
Hatua hiyo ya serikali ni ya kupongeza na kuonesha ni sikivu kwa kusikia kilio cha wananchi wake.
Maoni ya wadau ni kuwa serikali inapotaka kuamua jambo kama lilivyokuwa la kuweka tozo, ni lazima ishirikishe wananchi kupata maoni kabla ya kuchukua uamuzi ili isitokee athari.
Malalamiko yaliyokuwa yakitolewa kila kukicha kutoka kwa wananchi hao kilikuwa hakina afya kwa maendeleo ya nchi.
Tozo hizo sio tu zilikuwa zikiumiza wananchi, bali hata kampuni ambazo baadhi zilidiriki kutangaza jinsi zinavyoathirika na tozo hizo na kusababisha kushindwa kujiendesha.
Wadau mbalimbali pia, walikuwa wakitoa kilio cha tozo kwa kuwa waathirika wakubwa walikuwa wananchi wa kipato cha chini ambao kwa kiasi kikubwa hutumia simu kufanya miamala ambayo ilikuwa ikiathirika kwa tozo hizo.
Akitangaza hatua hiyo ya serikali, Waziri wa Fedha alifafanua kuwa marekebisho yanayofanyika ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote), kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote).
Pia wafanyabiashara (merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye kanuni za sasa na kusamehe tozo ya miamala kwenye utozaji wa fedha tasilimu, kupitia wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi Shilingi 30,000 na kupunguza gharama ya miamala, kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kufuatana na kundi la miamala.
Tozo hizo viwango vilishushwa kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu cha Sh. 10,000 hadi kiwango cha juu cha shilingi 7,000, viwango vyake vilianza kutumika Septemba 7, 2021.
Waziri Mwigulu ametangaza nia ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka kupunguzwa zaidi ya tozo na Wizara ya Fedha, ilipunguza tozo zaidi kwa kushusha tena kiwango cha juu kutoka 7,000 hadi 4,000.
Pamoja na kuwa kupunguzwa kwa tozo hizo kutapunguza mapato ya serikali, kama alivyoeleza Waziri wa Fedha, lakini kuna njia nyingi za kupata mapato badala ya kutegemea tozo pekee.
Vile vile, kuna matumizi ambayo yanaweza kupunguzwa kwa kubana matumizi ili serikali isiweze kuathiri katika utendaji wake wa majukumu ya msingi ya mafungu husika.
Waziri wa Fedha ameeleza maeneo yatakayotumiwa kubana matumizi hayo ni kuondoa bajeti ya chai, vitafunwa, misafara kwenye safari za ndani na nje kwa maofisa wa Wizara kama Rais Samia Suluhu Hassan, alivyoelekeza.
Kutokana na hatua hiyo, Waziri wa Fedha, amemwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali, kukaa na maofisa masuuli wote kuangalia upya mafungu ya matumizi mengineyo ili miradi ya maendeleo yote ithiathirike kwa hatua hiyo.