Upigaji fedha za miradi ya maendeleo ukomeshwe

22Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Upigaji fedha za miradi ya maendeleo ukomeshwe

KATIKA siku za hivi karibuni wakati viongozi mbalimbali wa kiserikali wakitembelea miradi ya maendeleo ya ujenzi, kumeibuka madai ya fedha kutumika ndivyo sivyo au kutoendana na gharama halisi za miradi yenyewe.

Viongozi hao wakiwamo wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na wa ngazi za juu, wanapotembelea miradi hiyo hubaini kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi hiyo.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alishangazwa na ujenzi wa kibanda cha mlinzi kutumia gharama kubwa kuliko uhalisia.

Huo ni mfano mmoja kati ya mingi inayojitokeza wakati viongozi wanapotembelea miradi hiyo.

Waziri Joyce Ndalichako, hivi karibuni naye alibaini ujenzi wa chuo kimoja kutumia gharama kubwa kuliko mradi wenyewe na kukosa majibu ya uhakika.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru pia anapotembelea miradi ya maendeleo, wakati mwingine hugoma kuizindua kutokana na kutoridhishwa na utekelezaji wake.

Hali hiyo huiibua Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini kuchunguza ubadhirifu wa mabilioni yanayotolewa na serikali kutekeleza miradi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Fedha nyingi zinazolalamikiwa kutumika vibaya ni pamoja na za UVIKO-19 ambazo zinatolewa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali.

Ukichunguza fedha hizo zinavyotumika ni kinyume na masharti yaliyotolewa na wafadhili na serikali katika utekelezaji wake.

Kwa mfano imeelezwa kuwa TAKUKURU imeanza uchunguzi wa mradi wa ukarabati wa Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu Sabasaba kilichopo mjini Singida.

Uchunguzi huo unatokana na agizo alilolitoa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, kwa TAKUKURU baada ya kutembelea chuo hicho na kubaini ubadhirifu mkubwa wa fedha uliofanywa na watendaji wa serikali.

TAKUKURU, ilipata taarifa za ubadhirifu katika chuo hicho na uchunguzi umeshaanza kufanyika.

Taarifa hizi za upigaji wa fedha za miradi hazipendezi kwa sababu zinarudisha nyuma juhudi za serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi wake.

Vile vile, ni aibu hata kwa wafadhili wanaotoa fedha hizo wakisikia kuwa zinatumika ndivyo sivyo.

Na watu wachache wenye tamaa na ubinafsi wasiharibu sifa ya nchi, hivyo hakuna budi watu hao wakashughulikiwa na kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo.

Ubadhirifu huo ni katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi ambavyo huongezwa bei kubwa kuliko uhalisia, kuweka makadirio makubwa ya mahitaji ya vifaa vya ujenzi (BOQ) na kutopelekwa kwa baadhi ya vifaa sehemu husika.

Kwa mfano matofali yakitakiwa 7000, watendaji wanaandika 14,700 na pesa inatolewa na kupigwa.

Bei ya saruji inawekwa kubwa Sh.18,000 bila kodi ya VAT na mifuko inayohitajika 2,912 wakati inayotakiwa kwa ajili ya kazi hiyo ni mifuko 900 pekee kwa mujibu wa mkandarasi, lakini pesa ikatolewa ya mifuko 2,912.

Upigaji mkubwa huwekwa kwenye vifaa vya ujenzi kwa kuongeza idadi kubwa kuliko mahitaji na bei pia ya kununulia huongezwa ili hao watu wachache waweze kujinufaisha.

Hizo ni sehemu tu ambazo watu hutumia mwanya wa kujinufaisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi.

Ziara hizi za viongozi ziendelee kuibua wabadhirifu hawa ili tabia hii iweze kukomeshwa.