Wananchi waelimishwe viashiria ukatili kijinsia

06Dec 2022
Mhariri
Nipashe
Wananchi waelimishwe viashiria ukatili kijinsia

MATUKIO ya ukatili wa kijinsia yanapotokea katika maeneo mbalimbali, baadhi ya wananchi hushindwa kuyatambua na kuyaripoti kwa sababu ya kukosa uelewa au elimu.

Kuna matukio ambayo hufanyika katika jamii, lakini anayefanya kitendo hicho au watu wanaomzunguka kushindwa kuelewa kama huo ni ukatili.

Ndiyo maana kunahitajika elimu ili watu waweze kuelewa matukio hayo yanapofanyika waweze kuyakemea.

Pengine kutokuwa na elimu ya uelewa wa matukio hayo husababisha kushamiri na kila mara yakisikika kwenye vyombo vya habari mbalimbali yakiripotiwa.

Matukio ya ukatili wa kijinsia mengi yao yanafanywa na watu wa karibu. Inaposikika kuripotiwa mtoto amefanyiwa ukatili wa kunajisiwa, ikifuatiliwa itagundulika aliyemfanyia hivyo ni mjomba, baba wa kambo na wakati mwingine ni baba mzazi.

Kumekuwa na mtukio kadhaa pia ya watoto wa shule kufanyiwa ukatili wa kingono wanapokuwa wanakwenda shule na kurudi nyumbani kwa kutumia usafiri wa mabasi ya shule.

Watu wanaowafanyia ukatili huo ni wale wanaoaminiwa na wazazi na walimu, yaani makonda na madereva wa magari hayo.

Juzi juzi tu kumeripotiwa tukio la mwanafunzi kufanyiwa unyama wa kuchangiwa na konda na dereva kwa kuwa huwa wa kwanza kuchukuliwa na wa mwisho kurudishwa nyumbani na kufanyiwa unajisi huo.

Wazazi kwa kutofuatilia kwa imani ya watu waliowakabidhi watoto wao, hawawachunguzi au kuongea nao kujua maendeleo yao na watoto hao kwa kuwa hutishwa na wanao wafanyia vitendo hivyo, huogopa kuwaambia wazazi.

Inakisikitisha na kuumiza pale mzazi anapokuja kugundua mtoto akiwa ameshaharibika na wengine kupata ulemavu wa maisha.

Ndiyo maana kuna umuhimu mkubwa wa kuwapo kwa elimu itakayohusisha jamii nzima kufahamu matukio ya ukatili yanapotokea na kuyakemea ili yasiendelee kuwapo.

Katika baadhi ya nyumba vitendo hivyo hutokea na pengine majirani wanashuhudia, lakini wanashindwa kuwajulisha wazazi kwa kutokuwa na ushirikiano au ukaribu.

Wengine wanashindwa kuelewa ukatili wa kijinsia ni upi ili unapotokea mtu aweze kuuripoti.

Baadhi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ni vipigo, ukeketaji kwa watoto, unyanyasaji wa aina yoyote ikiwamo wasaidizi wa ndani kupewa kazi kubwa kuliko uwezo wao na kunyimwa chakula.

Hivyo ni baadhi tu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na mtu yeyote anapoona vinafanyika katika eneo lake analoishi au kwa jirani yake anapaswa kutoa taarifa, ili kunusuru mhusika asiendele kupata mateso zaidi.

Katika kipindi cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, elimu na shuhuda mbalimbali zimekuwa zikitolewa ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, anasema mitandao ya kijamii ina mchango mkubwa katika kupunguza ukatili wa kijinsia ikiwamo kufichua unyanyasaji wanaofanyiwa watu majumbani.

Vilevile, mitandao ya kijamii inasaidia taasisi, wanaharakati na serikali kupata takwimu ya uwapo wa matendo hayo ikiwamo aina za unyanyasaji wa kijinsia inayofanyika na mikoa ambayo matendo hayo yanafanyika sana.