Simba, Yanga jiimarisheni kimataifa dirisha hili dogo

05Dec 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga jiimarisheni kimataifa dirisha hili dogo

WIKI ijayo Desemba 15, dirisha dogo la usajili kwa Klabu za Ligi Kuu, Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) na First League (zamani Ligi Daraja la Pili) litafunguliwa rasmi kwa ajili ya timu kujiimarisha tayari kwa raundi ya pili ya ligi zao.

Hata hivyo, kuelekea kufunguliwa kwa dirisha hilo ni fursa nzuri pia kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu, Simba na Yanga.

Wawakilishi hao, Simba wanaipeperusha bendera ya taifa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo kwa sasa wanasubiri kufahamu wapinzani wao watatu watakaopangwa nao hatua ya makundi wiki ijayo.

Kwa upande wa Yanga, yenyewe ina jukumu la kuiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, pia wiki ijayo itafahamu wapinzani wake watatu katika hatua ya makundi wakati droo hiyo itakapofanyika jijini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya CAF.

Hivyo, wakati zikisubiri droo hiyo, kinachotakiwa kwa sasa ni kila moja kuanza kumulika wapi pakujiimarisha zaidi ili kwenda kufanya vizuri katika michuano hiyo ambayo inaingia hatua ya makundi yenye ushindani mkubwa zaidi.

Tunaamini mabenchi ya ufundi ya klabu hizo yameshawasilisha ripoti zao kwa kamati zao za usajili kwa kumulika nafasi ambazo wanahitaji kufanyiwa maboresho zaidi kuelekea usajili wa dirisha dogo wiki ijayo.

Kwa maana hiyo, kilichobaki ni viongozi na kamati zao za usajili kutimiza malengo hayo kwa kusajili nyota wakuja kucheza na kutoa ushindani kuanzia ndani ya vikosi vyao na kuzisaidia timu zao kwenye mashindano husika na si kuongeza wakukaa benchi.

Pamoja na ukweli kwamba tunatambua katika usajili wa dirisha dogo ni vigumu kupata wachezaji wazuri kutokana na wengi mikataba yao kumalizika mwishoni mwa msimu na hata wakipatikana huwa ni kwa gharama kubwa kutokana na klabu zao kuhofia kukosa mbadala wa kuziba nafasi zao, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu dhamira ya kweli ikiwekwa.

Licha ya changamoto hizo, tunaamini hakuna namna zaidi ya viongozi wa klabu hizo kukubali 'kuvunja benki' zao ili kusajili wachezaji watakaoweza kuwapa mafanikio katika michuano iliyo mbele yao.

Sisi tunaamini kwa ubora ambao wawakilishi wetu hao wameonyesha hadi kutinga hatua ya makundi, pakifanyika maboresho yenye tija katika usajili wa dirisha dogo, wawakilishi hao wa nchi wanaweza kutinga nusu fainali hata fainali.

Malengo yetu ni kutaka kuona wawakilishi hao wote kwa pamoja wakifika hatua hiyo kubwa na si kuishia hapo tu bali pia kutwaa mataji hayo ili kujenga heshima ya soka la Tanzania.

Lakini hayo hayawezi kutimia kama utafanyika usajili wa mazoea, wakusubiri wachezaji ambao mikataba yao imemalizika na kutupiwa virago na klabu zao za awali.

Tunataka kuona wakisajiliwa watu wa kazi wenye viwango vinavyoeleweka na uzoefu wa michuano ya kimataifa kwani kufika hatua ya nusu fainali ama fainali kunahitaji wachezaji wenye kariba hiyo na uzoefu wa mashindano makubwa ya kimataifa, jambo ambalo tunataka kuliona katika dirisha hili dogo.