Mchezaji au timu inayofanya mazoezi kwenye uwanja wenye sifa, huchangia kukuza kipaji na ubora wake, na mwisho wa siku, matokeo chanya yanayotarajiwa hupatikana.
Huwezi kuona timu inafanikiwa kwa kutofanya maandalizi yake kwenye viwanja vyenye sifa zinazostahili, na endapo ikatokea hivyo, basi itakuwa imebebwa au wamebebwa na neno bahati.
Ni kweli bahati huchukua nafasi katika michezo kwa sababu katika upande wa soka tumewahi kushuhudia timu inayotawala mpira kwa muda mrefu, ikashindwa kufunga mabao pale wanapotengeneza nafasi, na mpinzani wake akawa makini kwa kutumia vyema nafasi moja au mbili ilizopata, ikaibuka na ushindi.
Idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, hazija viwanja vyake binafsi, baadhi hutumia viwanja vya kukodi vinavyomilikiwa na taasisi mbalimbali na klabu nyingine zenyewe hutumia viwanja vya shule, hali ambayo husababisha kusimama kwa programu za mazoezi pale wamiliki wanapokuwa na shughuli zao binafsi, au wanapokuwa wametoa ruhusa kwa watu wengine kutumia viwanja hivyo.
Hongera kwa Azam FC, Ihefu SC, JKT Tanzania, Mtibwa Sugar, Fountain Gate Academy, Gwambina FC na wengine ambao wamejaribu kujenga viwanja vyao kwa ajili ya kutumia kwenye michezo yao ya nyumbani.
Wakati kukiwa na kanuni maalumu inayozitaka timu zinazoshiriki kuwa na viwanja vyake, kanuni hiyo ikiwa na zaidi ya miaka mitano sasa, bado zipo klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara au Ligi ya Championship, zikiwa hazina hata uwanja wa mazoezi, hali ya kuwa biashara yake kubwa ni kucheza mpira.
Ni ngumu kwa timu kupata mafanikio wakati mambo ya msingi ambayo yamekuwa yakinadiwa na viongozi pale wanapokuwa kwenye kampeni wakijinadi watajenga viwanja, wengine wakidiriki kutaja na siku atakazoleta mabadiliko, kwa kukosa kitendea kazi muhimu.
Kama Ihefu na Gwambina zimeweza kujenga uwanja, kwa nini timu nyingine zinashindwa kupambana kuhakikisha zinapata miundo mbinu hiyo na kujiondoa katika gharama ya kulipia viwanja vya kukodi?
Umefika wakati viongozi waliopewa dhamana ya kuzisimamia klabu hizi wakatimiza ndoto za wanachama na mashabiki wao kwa kuacha alama siku watakayoondoka, kwa kujenga viwanja ambavyo vitasaidia kuendeleza wachezaji wao kuanzia wa timu za watoto hadi wakubwa, alama ambayo itabakia kwenye vitabu vya kumbukumbu vya klabu hiyo husika kwa muda wote.
Pia tunalikumbusha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kukaa tena na wadau wanaomiliki viwanja kuingia mikataba maalumu itakayosaidia timu au shirikisho hilo kufanya matengezo yatakayosaidia kuboresha viwanja husika na kutimika kwa michezo yote.
Kukosekana kwa viwanja bora mikoani, kunawanyima haki mashabiki wa timu husika kuzishangilia na kuwashuhudia wachezaji wao mubashara wanapocheza na badala yake, timu hulazimika kuhamia kwenye kiwanja kingine kilichoko mkoa wa jirani kucheza mechi zake za nyumbani.
Mbali na kupoteza haki ya kuwa nyumbani, lakini timu hukosa mapato kwa sababu huonekana kama mwenyeji naye yuko ugenini, tukae chini upya tufanyie kazi utekelezaji wa maboresho ya viwanja kwa vitendo na si kutoa taarifa za kufungia viwanja.
Huku umaarufu wa mchezo wa ngumi ukirejea kwa kasi, bado hali imekuwa ni mbaya kwa mabondia wa hapa nchini kufanya mazoezi katika maeneo ambayo si rasmi ambayo hayawasaidii kwenye kujiimarisha vizuri. Lakini mazingira hayo hayavutii kupata mabondia chipukizi kwa sababu ya uchakavu wa vifaa au maeneo ambayo hutumika kujifua.
Tatizo hili pia liko kwa wanariadha, hawa ndio wanakosa sehemu sahihi za kufanyia mazoezi kulingana na mchezo wanaoshiriki, ama wanafanyia mazoezi barabarani au kwenye sakafu ambazo hazina ubora unaotakiwa kufuatana na mchezo wao.
Bila miundo mbinu sahihi, bado safari ya mafanikio kwa wanamichezo nchini itaendelea kuwa ngumu hata kama watapata makocha na vifaa vyenye ubora.









