Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mguto, katika tathmini yake ya mzunguko wa kwanza amesema kuwa kila kitu kimekwenda vizuri na hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji na hata klabu kuhusu kucheleweshewa malipo yao, lakini changamoto kubwa imekuwa suala zima la waamuzi.
Katika ligi hiyo ambayo inaingia mzunguko wa pili, Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo baada ya kujikusanyia alama 38 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 35 moja mbele ya Simba inayoshika nafasi ya tatu, baadhi ya waamuzi walionekana kuwa tatizo katika kuzitafsiri sheria 17 za soka ama kwa kutojua au kwa dhamira yao mbaya wenyewe, jambo ambalo lilikuwa kero raundi ya kwanza.
Hadi mzunguko huo unakamilika, timu ya Polisi Tanzania ndiyo inayoburuza mkia ikiwa na alama tisa ikifuatiwa na Ruvu Shooting na Ihefu FC zenye pointi 11 katika nafasi ya 14 na 13, hivyo kwa ligi hiyo inaelekea katika raundi ngumu zaidi, jambo ambalo suala la waamuzi kuvurunda linapaswa kumulikwa zaidi.
Ni ukweli usiopingika waamuzi wa soka nchini wamekuwa chanzo kikubwa kwa baadhi ya timu kumaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi zisizostahili. Katika hilo, zipo zilizonufaika kwa kuzawadiwa pointi ambazo zimezifanya kumaliza nafasi za juu, lakini kuna baadhi ambazo zimeporwa alama zao na kujikuta zikimaliza mzunguko wa kwanza kwa kushika nafasi za chini ama za kati.
Hiyo inamaana kama huu ndio ungekuwa mzunguko wa pili, baadhi ya timu zingeshuka daraja ama kwenda kucheza mechi za mchujo 'play off ' kutokana na maamuzi mabovu ya baadhi ya waamuzi, lakini hata bingwa angepatikana pasipo haki kutendeka.
Kwa kuthibitisha hilo, tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa TPLB, pamoja na kamati zake ikiwamo cha Chama cha Waamuzi nchini (FRAT), imeonyesha meno yake kwa kuwafungia baadhi ya waamuzi waliobainika kufinyanga sheria 17 za soka.
Hivyo, kuelekea mzunguko huu wa pili wiki hii pamoja na TPLB kukiri kuwapo tatizo, waamuzi hawana budi kujitathmini zaidi na kugeukia katika kutenda haki na ionekane kweli ikitendeka ili ligi yetu izidi kuwa bora na kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Si hilo tu, bali pia waamuzi wakichezesha kwa haki tutapata wawakilishi bora wa nchi kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu Afrika, ambazo zitabeba jukumu la kwenda kuipeperusha bendera ya Tanzania.
Hivyo, TFF, TPLB na FRAT hawana budi kuongeza makali zaidi kwa waamuzi wanaozifinyanga sheria 17 za soka kwani lengo letu ni kutaka kuona anapatikana bingwa aliyestahili na hata timu zinazoshuka daraja na zile za kucheza mechi za mchujo kuwania kubaki na kupanda Ligi Kuu, ziwe zile zilizostahili kutokana na maamuzi bora na si vinginevyo.
Tunaamini maamuzi mengi ya ovyo yanayofanywa na waamuzi wetu si makosa ya kibinadamu kama mara kadhaa inavyodaiwa, bali wanadhamiria kwa sababu zao binafsi, hivyo mzunguko huu wa pili TFF na TPLB zisilale maana ndicho kipindi ambacho uvurundwaji mkubwa hufanyika.
Lakini umefika wakati wa waamuzi wetu kujitathmini wenyewe kwamba wanatosha kuifanya kazi hiyo na kuanza kubadilika ili kuwa miongoni mwa wale wanaopewa nafasi mara kwa mara ya kuchezesha michuano ya kimataifa kama zilivyo nchini jirani za Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan.










