Wadau hao wameona umuhimu na wajibu wa kutafuta ufumbuzi na kushughulikia sababu za unyanyasaji huo shuleni na nyumbani ili kuhakikisha watoto wanalelewa kwenye mazingira salama.
Kadhalika walimu wana nafasi kubwa ya kukomesha vitendo vya kikatili dhidi ya watoto shuleni ikiwa watashirikishwa kwa kupewa taarifa sahihi na mbinu za kutumia ili kuwajengea watoto uwezo wa kutambua ukatili na kutoa taarifa utakapojitokeza.
Pamoja na kuwekwa kwa madawati ya jinsia katika maeneo muhimu ili wananchi waweze kutoa taarifa vitendo vya ukatili vinapojitokeza, lakini kuna baadhi ya watu wanakosa uelewa au elimu ya kuripoti matukio hayo.
Katika baadhi ya mitandao ya kijamii, kuna video fupi inayomwonesha askari polisi akiwafundisha watoto jinsi ya kujiepusha na watu wanaowafanyia ukatili wa kijinsia.
Askari huyo anawaonesha watoto namna ya kukataa iwapo watu watawashika maeneo nyeti na kuwaripoti mara moja.
Kwa kweli hatua ya askari huyo kujitoa kuwafundisha wanafunzi ni ya kuungwa mkono na watu wengi zaidi ili watoto wasiendelee kukumbwa na vitendo hivyo ambavyo huwaharibia ndoto zao za kufika mbali kielimu.
Kuna matukio ambayo hufanyika katika jamii, lakini anayefanya kitendo hicho au watu wanaomzunguka kushindwa kuelewa kama huo ni ukatili.
Ndiyo maana kunahitajika elimu ili watu waweze kuelewa matukio hayo yanapofanyika waweze kuyakemea.
Matukio ya ukatili wa kijinsia mengi yanafanywa na ndugu wa karibu.
Kumekuwa na mtukio kadhaa pia ya watoto wa shule kufanyiwa ukatili wa kingono wanapokuwa wanakwenda shule na kurudi nyumbani kwa kutumia usafiri wa mabasi ya shule.
Watu wanaowafanyia ukatili huo wanaaminiwa na wazazi na walimu.
Inakisikitisha na kuumiza pale mzazi anapokuja kugundua mtoto akiwa ameshaharibika na wengine kupata ulemavu wa maisha.
Katika baadhi ya nyumba vitendo hivyo hutokea na pengine majirani wanashuhudia, lakini wanashindwa kuwajulisha wazazi kwa kutokuwa na ushirikiano au ukaribu.
Baadhi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ni vipigo, ukeketaji kwa watoto, unyanyasaji wa aina yoyote ikiwamo wasaidizi wa ndani kupewa kazi kubwa kuliko uwezo wao na kunyimwa chakula.
Mtu yeyote anapoona vinafanyika katika eneo lake analoishi au kwa jirani yake anapaswa kutoa taarifa, ili kunusuru mhusika asiendele kupata mateso zaidi.
Katika kipindi cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, elimu na shuhuda mbalimbali zimekuwa zikitolewa ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, anasema mitandao ya kijamii ina mchango mkubwa katika kupunguza ukatili wa kijinsia ikiwamo kufichua unyanyasaji wanaofanyiwa watu majumbani.
Vilevile, mitandao ya kijamii inasaidia taasisi, wanaharakati na serikali kupata takwimu ya uwapo wa matendo hayo ikiwamo aina za unyanyasaji wa kijinsia inayofanyika na mikoa ambayo matendo hayo yanafanyika sana.









