Tayari maeneo ya huduma za jamii kama shule, vyuo, zahanati na vituo vya afya vimezingirwa na maji kiasi cha kushindwa kutumika, huku makazi ya watu yakiharibiwa vibaya.
Ziwa hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani likiwa mpakani mwa Tanzania kwa asilimia 46, huku sehemu ikiwa Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo asilimia 40, kote shughuli za uvuvi wa mazao ya samaki yanafanyika ambao umekuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kutokana na kuongezeka kwa maji mwalo wa Kibiziri, Kigoma Ujiji umefunikwa kiasi kwamba wafanyabiashara wa dagaa na samaki hawawezi kuendelea na shughuli zao, wametawanywa kwenye maeneo mengine ili waendelee kujitafutia mahitaji.
Wengi maisha yao yamebadilika kwa kuwa wamelazimika kuanza kutumia mitaji yao, kujifunza shughuli nyingine kama kuuza maandazi na kushona mashuka, baadhi wanasema wameshindwa kusomesha watoto wao kwa kuwa fedha wanayopata inatosheleza mlo mmoja kwa siku na siyo kununua madaftari, sare za shule, viatu na mabegi.
Wanawake wajasiriamali wameeleza maisha yao kuwa kabla ya kuongezeka kwa maji waliuza dagaa au samaki kwa Sh. 40,000 hadi 60,000 na kupata kati ya Sh. 5,000 hadi 20,000 kwa siku ambayo iliwasaidia kuboresha maisha yao.
Kwa sasa wapo wanaoingiza Sh.2000 kwa siku ambayo hutumiwa na familia kupata mlo mmoja ambao huliwa saa 10 jioni, huku wengine hawana uhakika wa kupata hata Sh.100.
Pia kutokana na mabadiliko ya tabianchi, idadi ya samaki imepungua, huku wakilazimika kuwafuata mbali hali inayopandisha bei na wengi kushindwa kuendelea na biashara hiyo kama ajira.
Shughuli za kiuchumi za mkoa wa Kigoma ni uvuvi na kilimo, wengi wakitegemea ziwa hilo kukua kiuchumi hasa kwenye kuuza samaki na dagaa, lakini hali inavyokuwa hivyo ni hasara na wengi wanarudi kwenye umaskini.
Mabadiliko ya tabianchi si tukio la kushtukiza bali hutokea taratibu huku kukiwa na viashiria vingi, ambavyo kwa jamii iliyoelimishwa ni rahisi kutambua na kuchukua hatua.
Tunatambua kuwa mabadiliko hayo ni suala la kidunia, lakini jamii na nchi inaweza kufanya jitihada za kutunza mazingira kiasi cha kurejesha ubora wake, lakini wanaweza kujiandaa mapema kuwa na shughuli mbadala.
Mathalani, taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na watafiti mbalimbali zinaweza kuwafikia wananchi katika ngazi ya chini kabisa, ili wanapofanya maamuzi ya kulima mazao fulani au kuendelea na shughuli fulani wajue mabadiliko yaliyoko.
Kila jamii ina namna ya kutambua viashiria vya hatari kwenye maeneo yao, baadhi wakitumia wazee wa zamani kuwaeleza historia ya eneo na kujua kikitokea kitu fulani ni dalili ya jambo fulani kutokea, ili wajue hatua za kuchukua.
Ni muhimu wananchi wakafundishwa ikiwamo kuwa na shughuli mbadala ili yanapotokea mabadiliko kama haya au majanga mengine waweze kuendelea na maisha, hili ni jukumu la serikali kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi.
Tunajua serikali imeridhia mikataba mbalimbali ikiwamo Sendai Frame Work, kwa ajili ya nchi kuwa na mikakati ya kukabili majanga pamoja Malengo Endelevu ya Milenia (SDGs).