Waamuzi bado kikwazo ushindani Ligi Kuu nchini

24Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Waamuzi bado kikwazo ushindani Ligi Kuu nchini

KADRI muda unavyozidi kusonga mbele Ligi Kuu Bara inazidi kuwa ngumu, lakini na kuwa kivutio kikubwa kwa watazamaji na si Tanzania pekee, bali katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na imeonyesha wazi inastahili kabisa kushika nafasi ya nane kwa ubora barani Afrika.

Kwa sababu hiyo hatutachoka kulipongeza Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB), wadau wote wa soka hususan wadhamini kuanzia wale wa ngazi ya klabu hadi wa ligi hiyo pamoja na mashabiki wote kwa kuunga mkono juhudi hizo.

Ni wazi TFF na TPLB wametumia na kubwa kuwashawishi wadhamini hadi kuandika historia kwa mara ya kwanza tangu ligi hiyo kuanzishwa nchini kuwapo kwa wadhamini wakubwa zaidi ya watatu waliokubali kudhamini Ligi Kuu kwa mabilioni ya shilingi.

Na taratibu sasa mashabiki wa soka nchini wanaonekana kuvutiwa zaidi kutazama mechi za Ligi Kuu nchini na kusahau ligi pendwa duniani ya kama England, Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa au wakati mwingine inapolazimu huangalia zote kwa pamoja, hakika si kazi ya mchezo iliyofanywa katika kuiboresha na kuwa na mvuto.

Lakini hilo limechangia pia kuwavutia wageni wengi kuja kucheza soka nchini, na si Ligi Kuu tu bali hata Ligi Daraja la Kwanza (Championship) kwa sasa wamesajiliwa huko na kuongeza ushindani na viwango vya wachezaji wazawa.

Kutokana na uwapo wa wageni kumesaidia kwa asilimia kubwa kuongezeka kwa ubora wa wachezaji wazawa jambo ambalo litakwenda kuongeza kitu katika timu zetu za taifa, kuanzia zile za vijana hadi wakubwa, Taifa Stars.

Hiyo ni kutokana na wachezaji wetu wengi wanaunda timu za taifa kucheza soka la ndani, jambo ambalo halitoi fursa kwao kuweza kujifunza mbinu nyingi kutoka kwa wachezaji wenzao ama makocha wa kigeni.

Na katika hilo, pia tumeshuhudia zaidi ya asilimia 90 ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zikinolewa na makocha wa kigeni, kitu ambacho pia kinatoa fursa kwa wachezaji wetu wazawa kujifunza mambo mengi, hivyo tunaamini huu ni mwanzo wa kupata matokeo chanya kwa timu zetu za taifa.

Uwapo wa wachezaji kutoka Senegal, Mali, Ivory Coast na makocha kutoka Tunisia, Hispania, Brazil na Afrika Kusini ni wazi kuna kitu wachezaji wazawa watanufaika nacho hususan kimbinu na kiufundi, hivyo ni wakati wa kuzidi kuhamasisha wageni zaidi kuja kufanya kazi nchini.

Wanaoweza kuongeza ama kuua kabisa hamasa hiyo kwa sasa ni waamuzi, ambao baadhi yao suala la kuchezesha soka kwa kufuata sheria 17 za soka duniani, limekuwa tatizo kubwa kwao, jambo ambalo linazua malalamiko kila wiki.

Kushindwa kumudu mchezo, kufanya kwa makusudi au kwa mapenzi binafsi ama pengine kwa kurubuniwa, kumekuwa kukiathiri sana mechi na kulitia doa soka letu, kitu ambacho tunaona kinaweza kuchangia kwa asilimia kubwa kudidimiza ukuaji na uwekezaji mkubwa ambao umeanza kufanywa na wadau wa soka.

Katika hilo, pia baadhi ya waamuzi wameshindwa kabisa kulinda afya za wachezaji uwanjani kwa kuachia rafu mbaya kuendelea mchezoni kitu ambacho tunaona kama wakiachwa bila kuchukuliwa hatua msimu huu unaweza usimalizike salama.

Hivyo, tunaona ipo haja sasa kwa TFF na TPLB, kutokawia kutoa adhabu kali kwa waamuzi kwa mujibu wa kanuni, ili kulinda ubora wa ligi yetu na kuzidi kuvutia wageni kuja kufanya kazi nchini, lakini wawezekezaji kwa maendeleo ya soka letu.