Mechi hiyo ya Tanzanite Queens inayoongozwa na Kocha Mkuu, Bakari Shime dhidi ya Ethiopia itachezwa kesho kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tanzanite Queens ilifika hatua hiyo baada ya kuwaondoa Eritrea na baadaye Burundi ambapo katika mechi ya marudiano ilicheza ugenini Bujumbura ikiwa na wachezaji nane uwanjani kutokana na nyota wengine kukutwa na changamoto ya ugonjwa wa Uviko 19.
Wawakilishi hao wa Tanzania wamebakiza mechi tatu ili kupata tiketi hiyo ya kushiriki fainali hizo za Dunia, ambapo itakuwa ni kwa mara ya kwanza. Fainali hizo zitafanyika baadaye mwaka huu nchini Costa Rica.
Huu ni wakati mwingine muhimu kwa serikali, makampuni, taasisi na wadau mbalimbali wa michezo kuisapoti timu hiyo ili itimize malengo yake ya kupeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa.
Tanzanite Queens inakabiliwa na dakika 90 za nyumbani na nyingine kama hizo itakapokwenda Ethiopia. Ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, wadau wanatakiwa kukaa karibu na wachezaji wa timu hiyo kwa kuwapa motisha mbalimbali ambazo zitawaongezea nguvu ya kupambana kwenye michezo hiyo inayowakabili.
Tunaamini kwa upande wa ufundi, makocha wamefanya kazi yao ipasavyo na sasa wadau nao wanatakiwa kuwakumbuka 'mabinti' hawa ambao wanapambana kuhakikisha nchi inaweka historia kwa kupata tiketi ya kushiriki fainali hizo za dunia.
Ni ukweli unaofahamika timu hiyo haina udhamini hivyo, maandalizi yake yanakumbwa na changamoto mbalimbali kwa sababu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linahudumia pia timu nyingine za taifa huku pia ikiendesha mafunzo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya mchezo huo unaopendwa zaidi.
Tunayakumbusha makampuni na taasisi mbalimbali kuacha kusubiri mpaka pale Tanzanite Queens inapokwenda katika fainali za dunia na kuanza kuwapatia zawadi, muda sahihi wa kuishika mkono timu hiyo ni sasa wakati ikiendelea na maandalizi.
Inafahamika wachezaji hao wanahitaji vifaa vya michezo, mlo kamili, malazi bora lakini pia posho kwa ajili ya kujikimu mahitaji binafsi, jitokezeni kuwashika 'mkono' mabinti hawa ambao wamebakisha mechi chache kuweka rekodi ambayo Tanzania haijawahi kufikiwa.
Lakini tunawakumbusha wachezaji pamoja na changamoto wanazokutana nazo, wanatakiwa kuendelea kujituma kwa sababu mashindano haya ni daraja la kutangaza vipaji vyao.
Mawakala na makocha kutoka sehemu mbalimbali wamekuwa wakizifuatilia mechi zinazochezwa na mataifa yaliyobakia kwenye michuano hii ili kusaka nyota wa kuwasajili kwenye klabu zao. Hivyo wachezaji wasikatishwe tamaa na badala yake watumie michuano hii kujitangaza wakitarajia kuzivutia klabu nyingine za nje ya Tanzania au mataifa ya Ulaya.
Tunaamini mpira wa miguu umesaidia kuwapa ajira wachezaji hawa wanawake kama ilivyo kwa kaka zao, lakini ikumbukwe bila mzazi au mlezi kumpa nafasi au kuthamini kipaji cha binti huyu, mafanikio ya mchezaji huyo yatakuwa na milima na mabonde.
Umefika wakati jamii ikabadilika kwa kuendelea kuwapa ushirikiano wachezaji wanawake ili kufikia ndoto zao. Kwenye umoja na ushirikiano, hakuna ambaye atashindwa kufikia malengo yake.
Safari ya kuelekea nchini Costa Rica inawezekana, Mungu ibariki Tanzanite Queens, Mungu ibariki Tanzania.










