Matukio kadhaa yamekuwa yakiripotiwa kila uchao na vyombo vya habari na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mengi nchini, huku matukio mengi yakihusisha mauaji ya familia katika mazingira yanayoacha shaka kutokana na wanaofanya vitendo hivyo kutojulikana.
Kwa kutaja baadhi ya matukio hayo Januari 17, mjamzito na watoto wake wadogo wawili waliuawa kwa kuchinjwa ndani ya nyumba yao na watu wasiojulikana kisha kutokomea.
Lingine lililotokea wiki iliyopita ni la watu watano wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Zanka wilayani Bahi mkoani Dodoma kuuawa kikatili na watu wasiojulikana huku miili yao ikikutwa ndani ya nyumba yao ikiwa imeanza kuharibika.
Limo pia la watu watano wakiwamo mke na mume kwa kuhusika na mauaji ya wanandugu watatu waliokutwa wameuawa na miili yao kutupwa mto Jellys eneo la Buzuruga wilayani Ilemela mkoani humo.
Hakika mauaji haya ni ya kushangaza kutokana na kuhusisha watu wengi wa familia moja, kitu ambacho kinamaanisha kuwa si mauaji ya bahati mbaya, bali ni ya makusudi.
Katika hali hii hakuna sababu ya kulitupia mzigo Jeshi la Polisi pekee kutafuta suluhisho, bali jamii nzima inao wajibu wa kujitafakari na kuchukua hatua za kuleta ufumbuzi wa matukio haya.
Kitu cha kwanza ambacho tunapaswa kukifanyia tafakuri ya kina kama taifa, ni kwa nini watu wameondokewa na hofu ya Mungu kutokana na mafundisho ya dini kukataza binadamu kutoa uhai wa binadamu mwenzake. Katazo hilo pia limo kwenye sheria za dola ikiwamo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunaona kwamba hakuna sababu ya mamlaka zenye jukumu la kushughulikia jamii kama maofisa wa ustawi wa jamii kutokaa ofisini badala yake waende kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na njia sahihi za kutatua migogoro.
Wawahimize kuzitumia mahakama na vyombo vingine kama mabaraza ya ardhi badala ya kujichukulia hatua mkononi, ikiwamo kufanya mauaji, ambayo yana athari mbaya kwa jamii nzima.
Kwa upande wa viongozi wa dini, tunawakumbusha kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuwahubiria na kuwakumbusha wafuasi wao na jamii nzima kutenda matendo mema kama vitabu vitakatifu vinavyoelekeza, hivyo kuwa na hofu na Mungu.
Kadhalika, tunayakumbusha mashirika yasiyo ya kiserikali hususan yanayojihusisha na masuala ya haki za binadamu kijikita kupeleka elimu ya haki za binadamu katika maeneo yote ya nchi hususan vijijini, ambako matukio mengi ya mauaji yanatokea.
Tanzania tuna bahati ya kuwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo baadhi ya majukumu yake ni kukemea, kufuatilia matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu ya kutoa mapendekezo ya namna ya kuyashughulikia. Bila shaka tume itakaa kimya kuhusiana na matukio yanayoendelea ya kwamba bado yapo kwenye uchunguzi wa Polisi.
Msisitizo wetu kwa jamii ni kwamba ijenge utamaduni wa kuzitumia mahakama katika kushughulikia migogoro na badala ya kujichukulia sheria mikononi, ikiwamo kufanya vitendo vya mauaji ambavyo vinawaathiri hata watu wengine wasio na hatia hususan watoto.