Wiki ya Sheria ichochee mabadiliko kwenye jamii

27Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wiki ya Sheria ichochee mabadiliko kwenye jamii

MAADHIMISHO ya Wiki ya Sheria ambayo hufanyika kila mwaka yalizinduliwa Jumapili jijini Dodoma na Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, huku viongozi wa mahakama ngazi zote nchini wakitoa ushauri kwa jamii.

Ushauri ambao mahakimu na majaji wameusisitiza ni kuwataka wananchi kuhudhuria katika maonyesho hayo ili wazijue sheria na taratibu za kufuata katika kutafuta haki zao.

Wiki ya Sheria ina umuhimu mkubwa kwa jamii, kwa sababu ni sehemu sahihi ya wananchi kwenda kupata elimu inayotolewa kwa ajili ya kuwapa elimu kuhusu wapi pa kwenda kutafuta haki pamoja na hatua muhimu zinazotakiwa kufuatwa.

Kuna migogoro mingi sugu katika jamii yetu ikiwamo ya ardhi, ndoa, mirathi na mingine ambayo inashindikana kupelekwa kwenye vyombo vya sheria hususan kwenye mahakama kutokana na watu kukosa uelewa.

Kutokana na hali hiyo, na sisi tunawahimiza wananchi kwenda kupata elimu katika maeneo yaliyo karibu nao kabla ya maadhimisho hayo kumalizika ambapo yanafanyika maonyesho yakiambatana na elimu na ufafanuzi unaotolewa na wataalamu mbalimbali wa sheria wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na sheria pamoja na haki za binadamu.

Tunahimiza hilo kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa kuhusu wapi pa kwenda kupata haki na taratibu za kufuata, hivyo mwishowe kupoteza haki zao za msingi.

Ukosefu wa elimu hiyo pia umekuwa kichocheo kikuu kwa watu kuamua kujichukulia sheria mkononi, ikiwamo kufanya mauaji ya wengine na wakati mwingine kuamua kujiua.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Musphafa Siyani, akizindua Mahakama ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma juzi, alisema ni aibu wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kufanya mauaji ya kikatili, badala ya kutumia mahakama ili kupata haki zao na kuepusha migogoro inayosababisha vifo.

Mbali na kuwahimiza wananchi kwenda kujifunza pamoja na kuzitumia mahakama katika kudai haki, tunaona kwamba maadhimisho ya Wiki ya Sheria ni jukwaa muhimu la jamii kuzijadili sheria zetu, ili zile zisizoendana na wakati zifutwe hususan ambazo zinakwaza maendeleo na ustawi wa jamii.

Sheria za aina hii nyingi ni za zamani ambazo taifa lilizirithi kutoka kwa wakoloni na nyingine walizitunga wakati wa ukoloni kwa maslahi yao binafsi ili kuwasaidia kufanikisha utawala wao.

Hata Tume ya Jaji Francis Nyalali iliziainisha sheria 40 ilizoziita kandamizi na kupendekeza zifutwe ilipokuwa ikitafuta maoni ya wananchi kuamua kama Tanzania iendelee na mfumo wa chama kimoja cha siasa ama wa vyama vingi urejeshwe.

Sheria hizo nyingi bado zipo na zinaendelea kulalamikiwa na jamii, hivyo tunaona kwamba maadhimisho ya Wiki ya Sheria yawe jukwaa la kuzipigia kelele sheria hizo zifutwe, tukiunga mkono kauli ya Rais Mwinyi kuwa sheria nzuri ni kichocheo cha maendeleo ya uchumi wa nchi.

Kadhalika, tunakubaliana na wito wa kiongozi huyo kwa wanasheria Tanzania Bara na Zanzibar kuzipitia sheria zilizoko na kushauri zilizo kinzani kuboreshwa.

Bila shaka wanasheria watakuwa wameipokea changamoto hiyo na kuwa tayari kuifanyia kazi. Kwa upande mwingine, Tume ya Kurekebisha Sheria nayo tunaamini kwamba itatimiza wajibu wake wa kushauri sheria ambazo ni kinzani na zimepitwa na wakati kwa maendeleo ya nchi yetu.

Tunawashauri mahakimu na majaji kuendeleza kasi ya kushughulikia mashauri yaliyoko mahakamani ili wananchi wapate haki zao kwa wakati, ili wauone mhimili huo kuwa ni mahali sahihi pa kukimbilia kutafuta haki.